NA
SALOME MAJALIWA - JKCI
MADAKTARI
wa Hospitali za Rufaa nchini wameshauriwa kuwatuma mapema wagonjwa wa moyo katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pindi wanapowapima na kugundulika kuwa na ugonjwa huo
ili waweze kupatiwa matibabu mapema.
Rai
hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari
bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka JKCI Delila
Kimambo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo
nchini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo.
Dkt.
Delila alisema wagonjwa wa moyo
wanaotibiwa katika Hospitali mbalimbali hapa nchini rufaa yao huwa ni Taasisi
ya Moyo hivyo basi ni muhimu wagonjwa hao wakafika katika Hospitali hiyo kwa
wakati.
“Wagonjwa
wengi tunaowapokea mioyo yao huwa imechoka, kama wagonjwa hawa wangefika mapema kwetu wangepata matibabu madogo kuliko kupatiwa matibabu makubwa ya upasuaji
wa kifua au bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo”.
“Kutokana
na wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitalini ama kutokupata matibabu ya moyo kwa
wakati, tumeona tuwe na mafunzo haya hii itawasaidia madaktari wengi kupata ujuzi zaidi na kuweza kutambua wagonjwa kwa wakati”, alisema
Dkt. Delila.
Akizungumzia
kuhusu mkutano huo Dkt. Delila alisema
lengo ni kuwapatia madaktari ujuzi hususani wa namna ya kupima moyo kwa
kutumia mashine za ECHO na umeme wa moyo (Electrocardiography
– ECG).
Kwa
upande wake Daktari kutoka hospitali ya Amana Natalius Kapilima alisema mafunzo
hayo yamewasaidia kupata ujuzi utakaowawezesha kuwatambua wagonjwa wa moyo
kupitia vipimo vya ECHO na ECG.
Naye
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka hospitali ya Aga Khan Prof. Mustafa
Bapuma aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuona mbali na kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa madaktari. Kupitia
mafunzo hayo wataweza kutibu wagonjwa wa moyo kwa ustadi na ufanisi zaidi
kuliko hapo awali.
Mkutano
huo wa siku moja umeandaliwa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Kampuni ya Merck ambapo jumla ya
washiriki 80 kutoka Hospitali mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam walishiriki.
Mkurugenzi
wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Delila Kimambo akielezea jinsi mashine ya kupima moyo (Echocardiogram) inavyofanya kazi ya kutambua matatizo yaliyopo katika moyo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa
wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo Jijini Dar es Salaam.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini
Marekani Prof.Matthew Sackett akielezea jinsi mtambo wa Cathlab unavyotumika kutibu na kupima magonjwa ya moyo
wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo uliofanyika
leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya Madaktari wa Magonjwa ya Moyo kutoka
Hospitali mbalimbali za mkoa wa Dar es
Salaam wakifuatilia mada ya jinsi ya kumtambua mgonjwa mwenye matatizo ya moyo
kwa kupitia kipimo cha ECHO wakati wa Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa
kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.(PICHA NA GENOFEVA MATEMU – JKCI)
No comments :
Post a Comment