Saturday, August 18, 2018

SERIKALI KUTOA MILIONI 405 KUKAMILISHA CHUO CHA AFYA TABORA


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia akinamama waliojifungua katika wodi ya wazazi kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete Agosti 18, 2018.

 
NA TIGANYA VINCENT

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameahidi kuhakikisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 405.7 zilizobaki zinatolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa Chuo cha Afya cha Tabora ili kazi zilizobaki zimalizike na kianze kutoa mafunzo.

Alisema lengo ni kuhakikisha ikifika mwakani mwezi wa kwanza Chuo hicho kinaanza kutoa kozi ambazo zitasaidia kuongeza wataalamu wa kada mbalimbali za afya.

Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo leo mjini Tabora baada ya kukagua majengo ya Chuo hicho ambayo yamekamika asilimia 85 toka miaka mitatu iliyopita lakini bado hayajaanza kutumika katika utoaji wa mafunzo.

Alisema atakutana na viongozi wa Wizara ya Afya kwa ajili ya kuona jinsi ya kuleta fedha mapame za kukamilisha maeneo yaliyobaki na kufanyia ukarabati sehemu zilizoanza kuharibika kama vile vioo ambavyo vimeshaanza kupasuka.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba alisema mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa bilioni 3.295 na kiasi kilichobaki ni milioni 405.7.

Alisema mradi huo ulikuwa unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 15 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) asilimia 85.

Dkt. Kamba alisema kwa upande wa ADB ilishakamilisha malipo yake yote katika mradi wa ujenzi wa Chuo hicho na kazi zilizokwisha fanyika zimefikia asilimia 85 bado upande wa Serikali.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alimwomba Waziri Mkuu kusaidia ili majengo ya Chuo hicho yaanze kutumika kuliko kubaki bila wanachuo na kuwa katika hatari ya kuchakaa.

Alisema kuanza kazi kwa Chuo hicho kutasaidia kupunguza tatizo la watumishi katika Hospitali ya Kitete kwa kuwa wanachuo watakuwa wakiongeza nguvu wakati wa mafunzo kwa vitendo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua chumba cha upasuaji kilichojengwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete wakati alipotembela hospitali hiyo katika Manispaa ya Tabora, Agosti 18, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa maelezo mafupi leo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kwa ajili ya kuzungumza na watumishi na viongozi mbalimbali wa Manispaa na Ofisi yake.

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na wa Manispaa ya Tabora na viongozi mbalimbali leo ikiwa  ni siku ya mwisho ya ziara yake Mkoani humo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Chuo cha Afya katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete  Agosti 18, 2018.  Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.(PICHA NA VINCENT TIGANYA OFISI YA RAS TABORA)

No comments :

Post a Comment