KITENGO
cha Afya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA)
kimeweka udhibiti madhubuti wa kujikinga na usambazaji wa magonjwa
ambukizi ukiwemo ugonjwa wa Ebola.
Ugonjwa
wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola, husababisha homa kali inayoweza
kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni na sehemu
nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi karibuni umetangazwa kutokea nchini Kongo na kusababisha
vifo.
Akizungumzia
kuhusiana na mikakati hiyo ya kupambana na magonjwa ambukizi ukiwemo wa
Ebola, Afisa Afya Mfawidhi wa JNIA, Dk. George Ndaki amesema wanatoa
mafunzo kwa watumishi na wahusika wote wanaotumia kiwanja hicho katika
kujikinga na magonjwa hayo.
“Sisi
tumejiandaa vizuri na tumeshafanya jitihada zote tumeshatoa maelekezo, mafunzo
na kamati mbalimbali za kiwanja zimejipanga kudhibiti magonjwa yote ya
kuambukiza, ikiwemo sisi wenyewe kujikinga na kuwakinga na abiria wote
wanaotoka katika nchi hatarishi”, amesema Dkt. Ndaki.
Aidha
akizungumzia kuhusiana na utaratibu ambao Kiwanja kimeweka ili kuhakikisha
abiria wenye maambukizi wanapokelewa kwa tahadhari, ambapo wanapowasili na
ndege zinazotoka nje ya nchi zinazopakia abiria wanaosafiri kutoka katika nchi
zinazoshirikiana na Kongo hutakiwa kusafisha mikono kwa dawa maalum mara
waingiapo katika eneo la kuwasili
Pia
abiria hao wanapoingia katika lango la kuwasili la abiria kutoka nje ya nchi,
kumekuwa na mashine maalum inaangalia joto la mwili na likizidi nyuzi joto 38 wanamtaka
kutoa maelezo Zaidi ya afya yake.
“Abiria
wote wanapowasili hupita katika eneo maalum ambalo wote hutakiwa kuosha mikono,
lakini pia kuna mashine ambazo zimewekwa ili kuweza kuwatambua abiria ambao
wanawasili wakiwa na hali ya joto isiyokuwa ya kawaida mfano kuwa na joto la
juu sana kuanzia 38oC, ukiachana na hilo kuna fomu maalum ambazo
abiria wanapowasili hujaza na pia taarifa kutoka kwa rubani wa ndege kama kuna
abiria ana maambukizi kwenye ndege. Baada ya kumtambua mgonjwa basi atapitishwa
katika njia ya tofauti na abiria wengine na kupakiwa katika gari la wagonjwa na
kupelekwa Temeke Hospital,” amesema Dk. Ndaki.
Naye
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw.
Paul Rwegasha akitoa ufafanuzi juu taarifa za uwepo wa ugonjwa wa Ebola,
ameeleza kuwa tayari JNIA wanazo taarifa za mlipuko wa ugonjwa huo na taratibu
zote zimeshachukuliwa kwa kuwakagua abiria wanaotoka nje ya nchi.
“Kwanza
kabisa kwa abiria wote ambao wanatokea katika nchi ambazo zinasadikika kuwa na
maambukizi wanapowasili wanakuwa sanitized (wanaosha mikono na dawa maalum) ili
wasiweze kuleta maambukizi ndani, lakini pia tuna thermo scanners
(mashine ambazo zinaangalia hali ya joto la mtu) anapowasili ambapo tunapogundua
mgonjwa anamatatizo tunapeleka isolation (Chumba cha wagonjwa wa kipekee) na
baada ya hapo anapelekwa katika vyumba vya waonjwa waliotengwa katika hospitali
ya Temeke” alibainisha Bw. Rwegasha.
Katika
hatua nyingine Dk. Ndaki amesema mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote ambaye
amebainika kuwa na ugonjwa wa Ebola kupitia JNIA.
Dk
Ndaki ametaja namna ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola ni pamoja na kuepuka
kugusa damu, machozi, jasho, matapishi, kamasi, mkojo au kinyesi cha mtu mwenye
dalili za ugonjwa; pia mtu hatakiwi kugusa, kuosha au kuzika maiti ya aliyekufa
kwa Ebola; pia usiguse au kula wanyama kama popo, sokwe au swala wa msituni.
Dalili
za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na misuli, mwili kulegea,
kutapika, kuharisha, vipele ma kutokwa damu
“Natoa
wito tu kwa wananchi kuhakikisha wanafuata taratibu zote tulizoziweka ili
kuhakikisha kwamba hatupati mgonjwa yeyote katika nchi yetu. Kama kila mtu
atatekeleza wajibu wake kwa abiria kufuata taratibu, wanaosimamia masuala ya
afya wakitimiza wajibu wao, na Kiwanja kikitimiza wajibu
wake basi hakika magonjwa ya mlipuko hayataweza kufika katika nchi yetu”
alieleza Dkt. Ndaki.
No comments :
Post a Comment