Saturday, August 18, 2018

DKT. KIGWANGALLA KURUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI, JK AMTEMBEELA TENA MOI

  NA ANDREW CHALE, MOI

RAIS Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI,  hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena leo Agosti 16, 2018.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Dkt. Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8,2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15, 2018 katika wodi ya Taasisi Tiba ya  Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo Dkt. Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia nafuu  ya haraka ili aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani  huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 eneoa la Magugu Mkoani Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye.

 Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla kitengo cha mifupa MOI anapopatiwa matibabu alipomtembelea kwa mara nyingine jana.

 Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla kitengo cha mifupa MOI anapopatiwa matibabu alipomtembelea kwa mara nyingine jana.(PICHA NA ANDREW CHALE)

No comments :

Post a Comment