Mkuu
wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua mradi wa maji
Mbuyuni ambao ulikamilika mwaka 2014 lakina bado wananchi hawapati maji
kutokana na maji katika chanzo hicho kuwa na rangi mbaya, Brigedia Jenerali
Mwangela amemuagiza mhandisi wa maji wilayani humo kufaya utafiti wa chanzo
kingine haraka.
NA GRACE GWAMAGOBE, SONGWE
MKUU wa Mkoa wa Songwe
Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela jana jioni amehitimisha ziara yake ya
siku mbili Wilayani Songwe, ambapo amekagua miradi kumi ya maendeleo na kisha
kuzungumza na watumishi na watendaji wa taasisi mbalimbali zilizomo wilayani humo.
Brigedia Jenerali
Mwangela akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa wa Mkoa wa Songwe akiwemo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe wametoa maelekezo yaliyohusu kuboresha
utendaji kazi kwa watumishi wa Wilaya ya Songwe.
Amesema “nimegundua
kila ambacho alinieleza Mkuu wa Mkoa aliyestaafu kuhusu wilaya ya Songwe ni
sahihi, upungufu alio uona nami pia nimeuona, napenda kusema mlikuwa mnamuona
ni yeye Mkali ila mimi nasema alikuwa Mvumilivu”.
Brigedia Jenerali
Mwangela amesema hatosita kumsema na kumchukulia hatua mtendaji anayeenda
kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa umma hivyo basi watumishi hao
wabadilike na kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, watembelee na
kukagua miradi inayotekelezwa wilayani humo.
Aidha amempongeza Mkuu
wa Shule ya Sekodari ya Kanga wilayani humo ambapo alifanya ziara ya kushtukiza
na kuwakuta walimu wote wapo darasani wanafundisha na mwalimu mkuu huyo akiwa
anafundisha huku akisimamia ujenzi wa mabweni shuleni hapo, amemshauri mwalimu
huyo kutumia wataalamu wa ujenzi wa wilaya ili Kusimamia ubora.
Baada ya kutembelea
Daraja la Kikamba linalounganisha kata ya Kapalala na Gua, Brigedia Jenerali
Mwangela amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Songwe Kumsimamia mkandarasi ili aweze
kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa muda uliopangwa ambao ni Septemba 7,
mwaka huu.
Katika kituo cha Afya
Mbuyuni amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha ujenzi unapokamilika,
vifaa tiba, dawa na wataalamu wa Afya wawepo ili kituo hicho kianze kutoa
huduma kwa wananchi na meneja wa Tanesco kwa kushirikiana na Mkoa kuhakikisha
kituo hicho kitakapoanza kutoa huduma kiwe na umeme.
Brigedia Jenerali
Mwangela amemtaka mhandisi wa maji Wilayani humo kufanya utafiti wa haraka wa
chanzo kingine cha maji kwa ajili ya mradi wa maji Mbuyuni kwakuwa wananchi
wamekataa kuyatumia maji ya chanzo cha awali kutokana na maji hayo kuwa na
rangi mbaya.
Ameongeza kuwa
wataalamu waliofanya utafiti awali hawakutendea haki taaluma yao na hivyo
kusababisha hasara kwa serikali huku wananchi wakiendelea kupata kero ya maji
tangu mradi huo ukamilike mwaka 2014.
Brigedia Jenerali
Mwangela amemtaka Afisa Afya wa Wilaya ya Songwe kutoa elimu kwa wananchi ili
wajenge vyoo bora, elimu ya masuala ya lishe, pia ahamasishe upimaji afya zao
hususani kwa magonjwa yasioambukiza kama tezi dume, kisukari, VVU pamoja na
kufanya tohara.
Ameongeza kwa kuwataka
watunze mazingira na kuendelea kusimamia agizo la katazo la ukataji ovyo miti
kwa ajili ya biashara ya mkaa, aidha ameelekeza wananchi wanaruhusiwa kuvuna
miti katika maeneo maalumu yaliyotengwa na wakala wa huduma za misitu (TFS).
Kwa upande wake
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Mathias Nyange amewataka watumishi kuacha
utoro kwakuwa wengi wao ifikapo siku ya ijumaa hutoroka na kuelekea Mkoa wa
jirani walipoweka makazi yao.
RPC Nyange amesema,
“nitamshauri Mkuu wa Mkoa vikao viwe vinafanyika siku ya Jumamosi ili kufuta
utoro huu, nawashauri watumishi unapopangiwa kituo cha kazi ndio kwenu papende,
ufanye kazi kwa bidi”
Ameongeza kuwa
serikali inatukanwa kutokana na uzembe wa baadhi ya watumishi hivyo wajitume
wabadilike na wafanye kazi kwa ushirikiano hasa katika kumsaidia mwananchi
masikini apate maendeleo.
Wananchi wa Kata ya
Mbuyuni Wilayani Songwe wakijitolea shughuli mbalimbali za ujenzi katika Kituo
cha Afya Mbuyuni ambapo serikali kuu ilitoa shilingi milioni 400 na kituo hicho
kinatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya
Mbuyuni Wilayani Songwe, kituo hicho kilipokea shilingi milioni 400 kutoka
serikali kuu na kinatarjiwa kukamilika mwezi ujao.
No comments :
Post a Comment