Wednesday, August 1, 2018

Bilioni 30/- kuboresha hospitali za rufaa

PichaNashon Kennedy
SERIKALI imetenga Sh bilioni 30 za ujenzi wa miundombinu bora ya utoaji wa huduma katika hospitali za rufaa kwa mwaka huu wa fedha.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amesema hayo alipozungumza na viongozi wa mkoa wa Geita katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili huko.

Ametaja baadhi ya miundombinu inayotarajiwa kujengwa na serikali katika hospitali hizo kuwa ni vyumba vya dharura, upasuaji, majengo ya mama na mtoto, vyumba maalumu vya wagonjwa mahututi kwa watoto na watu wazima (ICU) na kumaliza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya.
Amesema Geita ni moja ya mikoa ambayo imeanza kunufaika ambapo imepelekewa watumishi 70 wakiwemo madaktari 16. Aliutaka uongozi wa mkoa wa Geita kuwapokea watumishi hao na kuwapa ushirikiano mkubwa ili watekeleze vyema majukumu ya utoaji tiba.
Kuhusu huduma ya mionzi (x-ray) alisema sasa serikali ina mpango kutumia mfumo wa teknolojia mpya ya 'Placement', utaratibu wa kuangalia mahitaji ya hospitali na kuita zabuni.
Alisema vifaa vya kisasa vitafungwa na serikali itachangia huduma na endapo vifaa vitaharibika litakuwa ni jukumu la mzabuni kuvitengeneza.
"Madaktari bingwa watakaa sehemu moja baada ya kuunganishwa mfumo ambapo mgonjwa atapigwa picha ya mionzi (x-ray) na tafsiri inatoka kupitia mfumo huo," alisema.
Kuhusu upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Dk Ndugulile aliwahakikishia Watanzania dawa zote muhimu 167 zipo za kutosha na kwamba hakuna changamoto ya dawa kwa sasa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Joseph Odero alisema mkoa wa Geita bado una uhaba wa watumishi wa kada ya afya hali inayofanya wagonjwa kusubiria huduma kwa muda mrefu kwenye vituo vya kutolea huduma. Alisema mkoa una upungufu wa watumishi 2,088 kati ya mahitaji ya watumishi 3,783 na waliopo kwa sasa ni 1,695, asilimia 44.8.
"Pia mkoa una vituo vichache vya huduma za afya, asilimia 16 na zahanati asilimia 17 ya malengo ya serikali ya kila kijiji/mtaa kuwa na zahanati na kila kata kituo cha afya," alisema.
Alisema kuna changamoto ya mwitikio mdogo wa jamii kuchangia damu katika kampeni mbalimbali zinazoendeshwa na mkoa huo.
Alisema hata hivyo, mkoa unajitahidi kufanya ukusanyaji damu salama unakuwa endelevu kwa halmashauri zote ili kukabiliana na upungufu wa damu salama, dawa muhimu na vifaa tiba vinaagizwa kwa wakati kulingana na mahitaji.
"Wajawazito wanaonwa kwa wakati muafaka na kupatiwa huduma stahiki, ikiwemo utoaji wa elimu ya afya kwa jamii na kuwahimiza kuhudhuria kliniki", alisema.
Alisema Januari hadi Machi mwaka jana, mkoa ulifanikiwa kukusanya chupa 1,913 za damu salama ikilinganishwa na lengo la chupa 4,406 katika kipindi cha Januari-Machi mwaka huu. Alisema hiyo ni sawa na asilimia 43 ya lengo lao ambapo mahitaji ya mkoa yalikuwa ni kukusanya chupa 17,627 za damu mwaka huu.

No comments :

Post a Comment