Wednesday, August 1, 2018

Lukuvi aonya bei, ubambikizaji urasimishaji ardhi

Picha
Na Francisca Emmanuel
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani) amesema suala la urasimishaji wa ardhi litasimamiwa na maofi sa wa ardhi wilaya badala ya madiwani na viongozi wa serikali za mitaa, huku akisisitiza kwamba gharama kwa kila kiwanja ni Sh 250,000 na siyo Sh 500,000 au 800,000.

Lukuvi aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua Rasimu ya Mipango Miji ya Jiji la Dar es Salaam uliowahusisha wadau mbalimbali wa mipangomiji, madiwani, wabunge, viongozi wa serikali na viongozi wa dini.
Alisema gharama ya upimaji wa ardhi kwa kila kiwanja ni Sh 250,000 badala ya Sh 500,000 na 800,000 zilizokuwa zinatozwa awali na baadhi ya kampuni za urasimishaji, ambazo amezipiga marufuku kuchangisha wananchi ili wawapimie ardhi.
Kampuni tatu zinatafutwa kwa kutokomea na fedha. Aidha, alisema suala la urasimishaji litasimamiwa na maofisa wa ardhi wa wilaya badala ya madiwani na viongozi wa serikali za mitaa ambao walikuwa wakishirikiana na kampuni hizo, hivyo kusababisha wananchi kutozwa gharama kubwa ya upimaji wa viwanja.
Alisema serikali imewapa wananchi fursa ya kurasimisha maeneo yao yaliyojengwa kwenye maeneo yasiyo rasmi ili kupatiwa hati. Waziri huyo wa Ardhi alisema urasimishaji wa ardhi umeanza katika mikoa mbalimbali na kwamba kumekuwa na kasoro nyingi ikiwemo wananchi kutozwa kuanzia Sh 500,000 hadi Sh 800,000 kwa kupima kiwanja kimoja cha mwananchi maskini aliyejenga kwenye eneo lisilo rasmi.
“Baada ya kuchunguza nimegundua kuwa gharama halisi haizidi shilingi 250,000 kupimiwa kiwanja kimoja na ili kampuni zishindane kupitia zabuni zitakazotangazwa na wilaya ni lazima wapime kwa bei hiyo,” alieleza.
Alisisitiza kuwa ni marufuku kwa kampuni za urasimishaji kuchangisha fedha kwa wananchi ili wapate kuwapimia viwanja kwa kuwa imeleta changamoto, ikiwamo kampuni tatu zilizochangisha fedha kwa wananchi ili kuwapimia viwanja na kutorokea kusikojulikana na kuahidi kwamba watawatafuta.
Kwa mujibu wake, wananchi wenyewe watapaswa kufungua akaunti katika mitaa yao ambayo itasimamiwa na wananchi wenyewe bila viongozi wa mitaa kujihusisha na fedha hizo, na malipo yatafanyika baada ya kazi kuthibitishwa na maofisa wa wilaya na ikikubalika kwamba gharama yake ni kiasi hicho, ndipo wananchi watakapochangia fedha kwa wapimaji.
Waziri huyo alisema ni marufuku kwa kampuni binafsi kwenda kuomba kazi au kupewa kazi mtaani badala yake waanzie wilayani ambako wataisimamia na kuwa kiungo kati ya warasimishaji na warasimishwaji.
Aidha, alizipiga marufuku kampuni kuchukua fedha za wananchi na kuziingiza katika kampuni zao pamoja na madiwani na viongozi wa mitaa ambao wamekuwa wakichukua fedha kwa kampuni zinazofanya urasimishaji wakidai kwamba watawapa kazi hiyo na matokeo yake wanataka fedha nyingine, na badala yake zinaingia kwenye gharama za watu wanaotakiwa kupimiwa maeneo yao.
“Kazi hazitatolewa na mwenyekiti wa mtaa wala diwani, bali zitatolewa wilayani hivyo kampuni zisiende kuwahonga wenye mitaa,” alisema Lukuvi. Alifafanua, “Watendaji wa ardhi kote nchini wasimamie urasimishaji huo, migogoro itakayotokea watawajibika na kwamba isitokee mtu yeyote kuweka alama ya X katika nyumba zilizojengwa kiholela labda watu waliojenga maeneo ambayo yanahifadhi ya barabara na misitu iliyosajiliwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.”
Katika hatua nyingine, Lukuvi amewatoa hofu wananchi kwamba hakutakuwa na ubomoaji wa nyumba wala kuwaondoa waliojenga katika maeneo holela, badala yake kutafanyika maboresho ili kuipa hadhi ardhi hiyo. Aidha, imesema kuwa endapo Rasimu ya Mipango Miji ya Jiji la Dar es Salaam (Masterplan) ikipitishwa, kiwanja kimoja kinaweza kuwa na wamiliki zaidi ya 10.

No comments :

Post a Comment