Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kwenye
Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam Julai 19, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekutana na Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Mbelwa Kairuki na
amempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya tangu aende huko.
Amekutana na Balozi Kairuki leo
(Alhamisi, Julai 19, 2018) katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay
jijini Dar es Salaam, na amemtaka Balozi huyo ahakikishe anaboresha
mahusiano
kati ya Tanzania na China.
“Ni lazima nikupongeze kwa namna
unavyoendelea kufanya kazi na unavyojitahidi kudumisha mahusiano na
China. Tunashukuru kwamba wageni wanaokuja hapa nchini kutoka China
wanatoa taarifa nzuri na jinsi unavyosaidia kuitangaza nchi yetu huko
nje.”
“Umefanya kazi nzuri ya
kuwaelekeza wawekezaji wa huko kwamba wakati tunaunda Serikali na
kutengeneza mfumo wa utawala, tuliamua kujenga kwanza mifumo imara na
kutambua fursa zetu tulizonazo ili baadaye Watanzania waweze kunufaika
na hizo fursa.”
Amesema kupitia utaratibu huo,
Serikali ilitaka Watanzania wamiliki ardhi ndipo mgeni apate, na kama
kuna uzalishaji wowote unafanyika basi Mtanzania awe wa kwanza
kunufaika, Serikali inufaike na mwekezaji naye anufaike.
“Tunakushukuru kwamba umesaidia
kuwaambia wachina watulie wakati Serikali ikirekebisha mifumo yake. Na
wao wameyaona mabadiliko hayo, kwani tumesimamia vita dhidi ya rushwa,
na wao walikuwa ni waathirika wakubwa, lakini pia tumeongeza
uwajibikaji. Watu wetu sasa wanawajibika kwenye viwanda na makampuni yao
na Watanzania kwa ujumla, wametambua umuhimu wa kufanya kazi ili waweze
kuishi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali hivi
sasa iko kwenye programu ya kutangaza utalii uliopo nchini hasa kwa
kuamua kuagiza ndege kubwa zitakazobeba watalii na kuwaleta moja kwa
moja hapa nchini.
“Sasa hivi tumepata wageni maarufu
kutoka nje ya nchi akiwemo Rais mstaafu wa Marekani, Mheshimiwa Barack
Obama na wachezaji maarufu duniani, kwa hiyo tunaendelea na mikakati
yetu ya kutangaza utalii huko nje.”
No comments :
Post a Comment