Wednesday, July 18, 2018

MSD YATAKIWA KUTUPIA JICHO KITUO CHA AFYA KEREGE KWA KUKIPELEKEA VIFAA TIBA

IMG_20180718_101632
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu ,Charles Kabeho ,akitembelea na kujionea shughuli za mapambano dhidi ya Ukimwi katika kituo cha afya Kerege ,Bagamoyo Mkoani Pwani.
IMG_20180718_101416
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ,Charles Kabeho akizindua kituo cha afya Kerege wilayani Bagamoyo.
IMG_20180718_091426
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama (kulia) akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alhaj Majid Mwanga (kushoto) wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika shule ya msingi Mapinga.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………….
 
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
BOHARI ya madawa (MSD), imeelekezwa kufanya jitihada za kupeleka vifaa tiba vitakavyokidhi mahitaji ,katika kituo cha afya Kerege kilichopo Bagamoyo, Mkoani Pwani ,ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa vifaa tiba .
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu ,Charles Kabeho alitoa rai hiyo ,Kerege wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akikagua na kujionea shughuli za mapambano dhidi ya Ukimwi katika kituo hicho .
Alieleza ,,adhma ya serikali ni kuona vituo vya afya vinaongezeka ,huduma za afya zinaboreshwa hivyo MSD ihakikishe inasambaza vifaa hivyo na madawa ili kuendana na malengo ya serikali .
Akizungumzia suala la ugonjwa wa Ukimwi ,aliitaka jamii kujitambua kwa kupima afya zao na ambao walishagundulika kuwa na VVU waendelee na dawa bila kupuuzia masharti ya waatalamu wa afya.
Hata hivyo Kabeho alisisitiza ,ukimwi bado upo hivyo kila mmoja anawajibu wa kujali afya yake na kupambana na maambukizi mapya.
Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Kerege ,mganga mkuu wa wilaya hiyo, Silivia Mamkwe alisema hadi sasa mradi huo umegharimu kiasi cha sh.milioni 561 ambapo mil.500 ni fedha kutoka OR-TAMISEMI .
“Kiasi cha sh.mil.44 ni mchango wa halmashauri ,mil.11.353 ni mchango wa wadau ,mil.4.147 wananchi na mil .1.5 kupitia nguvu kazi “.
Silivia alisema, lengo la mradi ni kuboresha huduma za afya ,dharura na upasuaji wa wajawazito ambapo huduma za upasuaji wa dharura zimesogezwa karibu na wananchi kupunguza vifo vya mama na watoto .
Alisema ,mradi ulianza kutekelezwa oktoba mwaka jana na kwasasa majengo matano ,miundombinu mitano vimekamilika kwa asilimia 100,huku wakitarajia kufikia wananchi 8,921#.
“Majengo mawili la kuhifadhi maiti na jengo la kufulia yamekamilika kwa asilimia 80” alifafanua.
Awali akipokea mwenge wa uhuru kutoka Kibaha Vijiji ,Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alhaj Majid Mwanga alisema ,mwenge huo utapitia miradi 12 iliyogharimu sh.bilioni 10.8.
Alhaj Mwanga alielezea, miradi miwili itakaguliwa na miradi kumi itawekewa mawe ya msingi.
Mwenge wa uhuru unaendelea na shughuli zake Mkoani Pwani ,ikiwa umefikia halmashauri ya saba kati ya tisa na wilaya ya tano kati ya saba za mkoani hapo.

No comments :

Post a Comment