Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.
Fidelice Mafumiko (aliyesimama) akitoa hotuba wakati wa kufunga mafunzo
ya siku tatu ya Usimamizi Salama wa Kemikali kwa wahitimu wa masomo ya
Shahada ya Uhandisi wa Sayansi ya Madini na Uchakataji Madini (B.Sc.
Metallurgy and Minerals Processing Engineering) wa Chuo cha Sayansi ya
Ardhi (CoES), Chuo Kikuu cha Dodoma, yaliyofanyika mkoani Dodoma.
Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Ardhi
(CoES), Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa William Mwegoha (aliyesimama),
akizungumza kabla ya Mgeni Rasmi wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu
kuhusu Usimamizi Salama wa Kemikali kwa wahitimu wa masomo ya Shahada ya
Uhandisi wa Sayansi ya Madini na Uchakataji Madini (B.Sc. Metallurgy
and Minerals Processing Engineering) yaliyofanyika Dodoma na kuandaliwa
na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kati, Mkoani
Dodoma.
Washiriki wa mafunzo ya Matumizi
Salama ya Kemikali yaliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali, Kanda ya Kati, wakifuatilia hotuba ya kufunga mafunzo hayo
iliyokuwa inatolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko
(hayupo pichani).
Kaimu Meneja wa Maabara ya Kanda
ya Kati, Bw. Musa Kuzumila, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya
Usimamizi Salama wa Kemikali kwa wahitimu wa masomo ya Shahada ya
Uhandisi wa Sayansi ya Madini na Uchakataji Madini wa Chuo kikuu cha
Dodoma.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.
Fidelice Mafumiko akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo mmoja wa
washiriki wa mafunzo ya Usimamizi Salama wa Kemikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.
Fidelice Mafumiko, akiwa pamoja na Mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Ardhi
(UDOM), Prof. William Mwegoha, watumishi wa Chuo, watumishi wa
Maabara
ya Kanda ya Kati na wahitimu walioshiriki mafunzo ya Usimamizi Salama wa
Kemikali mara baada ya kufunga mafunzo hayo.
………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali (GCLA) imejipanga kuanza kutoa mafunzo endelevu ya matumizi
ya kemikali katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili kuongeza uelewa wa
matumizi bora ya kemikali hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dodoma na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko alipokuwa
akifunga mafunzo ya siku tatu juu ya matumizi ya kemikali kwa jumla ya
wanafunzi 40 wa Chuo Kikuu cha Dodoma wanaosoma masomo ya Uhandisi wa
Uchenjuaji Madini.
Dkt. Fidelice amesema kuwa moja ya
kazi za Mamlaka hiyo ni kutoa elimu kwa wadau wa kemikali ili
kuwawezesha kufahamu matumizi bora ya kemikali yakiwemo ya uzalishaji,
usafirishaji, uuzaji pamoja na uhifadhi wa kemikali.
“Mafunzo ya masuala ya kemikali ni
ya muhimu hasa ukizingatia nchi yetu inaelekea katika uchumi wa viwanda
ambapo matumizi ya kemikali yataongezeka hivyo tunajipanga kuweka
mikakati bora ambayo itatuwezesha kutoa mafunzo ya kemikali chuoni hapa
kwa wanafunzi wanaosoma kozi zinazohusisha matumizi ya kemikali”,
alisema Dkt. Mafumiko.
Dkt. Fidelice ameongeza kuwa
uanzishwaji wa mafunzo ya kemikali katika chuo hicho ni mlango wa
mahusiano ya kitaaluma kati ya Mamlaka na chuo jambo ambalo litasaidia
kukuza uelewa juu ya matumizi ya kemikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa rai
kwa wanafunzi hao kuwa mabalozi wa matumizi bora ya kemikali katika
jamii zao pamoja na kuwa wataalam wenye uelewa na weledi juu ya matumizi
ya kemikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha
Sayansi ya Ardhi (CoES), Prof. Willium Mwegoha amesema kuwa wanafunzi wa
kozi hiyo ni wadau wakubwa wa kemikali kwa sababu kazi zao zinahusisha
matumizi ya kemikali.
“Tangu kozi hii ianze hatujawahi
kupata mafunzo ya aina hii hivyo tunaomba yaendelee na siku zijazo kwani
yana umuhimu mkubwa kwa wanafunzi hawa”, alisema Prof. Mwegoha.
Akiwawakilisha wanafunzi wenzie,
Hemed Omary amesema kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa wa matumizi ya
kemikali hasa katika masuala ya sheria ya usimamizi na udhibiti wa
kemikali pamoja na madhara ya kemikali kwa afya na mazingira.
No comments :
Post a Comment