Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dr.
Damas Ndumbaro akisisitiza jambo wakati akizindua mashindano ya vilabu
vya Kodi kwa Shule za Sekondari katika Tamasha la Majimaji
Serebuka linaloendelea Songea Mkoani Ruvuma
Baadhi ya wanafunzi wa shule za
sekondari mkoani Ruvuma wakifuatilia mashindano ya Vilabu vya Kodi kwa
shule za Msingi katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Songea
Mratibu wa Mashindano ya Vilabu
vya Kodi kwa Shule za Sekondari Mkoani Ruvuma Njovu Kilian (aliyesimama)
akifafanua jambo kwa wananfunzi. Wengine ni Mbunge wa Songea Mjini Mhe.
Dr. Damas Ndumbaro (katikati) na Mwakilishi wa Benki ya NMB.
……………..
Wanafunzi katika shule za
sekondari wanatakiwa kufahamu masuala na umuhimu wa kodi kutokana na
juhudi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imefanya katika kutoa elimu ya
msingi na sekondari nchini bure
Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa
Songea Mjini Mhe.Dr. Damas Ndumbaro wakati akizindua rasmi mashindano
ya vilabu vya kodi kwa shule za sekondari katika Tamasha la Majimaji
Serebuka linaloendelea Songea katika Mkoa Ruvuma.
Mhe. Ndumbaro amesema kwamba
kutokana na kukosa mtaala wa elimu ya kodi katika shule za sekondari,
Mkoa wa Ruvuma uliamua kuwa na mdahalo wa masuala ya kodi kwa shule za
sekondari ili wanafunzi waweze kufundishana kwani katika kuwasilisha
mada za masuala ya kodi wanafunzi wanajifunza na kufundishana.
“Samaki mkunje angali mbichi. Umri
wa vijana walio sekondari ni umri mzuri wa kuwaelimisha masuala ya
kodi”, alisema Dr. Ndumbaro na kuongeza kwamba wanafunzi wakifundishana
wenyewe kwa wenyewe wataelewa zaidi kuliko wanapofundishwa.
Mbunge huyo wa Songea Mjini
alisema kwamba wanafunzi wanatakiwa kufahamu kwamba gharama ya elimu ya
bure inayotolewa katika shule za msingi na sekondari, ujenzi wa viwanja
vya ndege, barabara, ununuzi wa ndege, na upatikanaji wa umeme katika
Mkoa wa Ruvuma wa gridi ya taifa kutoka Makambako zinatokana na kodi.
Aidha amewataka wanafunzi
kushiriki vizuri katika mdahalo huo bila kujali kwamba watashinda au la
kwani kwa kuweza kufikia hatua ya ushiriki tayari wote ni washindi
Mdahalo huo unaohusu mashine za risiti za kielektroniki na umeandaliwa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na waandaji wa
Tamasha la Serebuka.
Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu
kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Richard Kayombo amewataka
wanafunzi kuelimisha jamii inayowazunguka kuhusu masuala ya kodi kwani
kodi ndio pato pekee linaloiwezesha nchi kuhudumia wananchi wake.
“Sisi tutaendelea kutoa elimu kwa
kadiri ya uwezo wetu bila kuchagua na nyinyi tunawaandaa ili muweze
kutoa elimu kwa familia zenu, majirani zenu, wanafunzi wenzenu na jamii
nzima inayowazunguka”, alisema Kayombo.
Amewataka wanafunzi kudai risiti
wanaponunua bidhaa, kulipa kodi wakati wa kulipa kodi ukifika kwani
wanafunzi ni wafanya biashara na walipakodi watarajiwa.
Naye Mratibu wa Mashindano ya
Vilabu vya kodi katika Tamasha hilo kutoka TRA Njovu Kilian amesema
kwamba Mashindano hayo yamekuwa na mwamko mzuri kutokana na kuongezeka
kwa washiriki. “Mwaka jana tulikuwa na washiriki 22 lakini mwaka huu
tuna shule 32 ambazo zinashiriki”, alisema Njovu.
Pamoja na kushindana kuwasilisha mada pia kutakuwa na shindano la kuchora katuni inayohusu masuala ya kodi
Mashindano ya Vilabu vya Kodi
katika shule za Sekondari katika Tamasha la Serebuka yanashirikisha
shule za Sekondari 32 za Mkoa wa Ruvuma ambapo baada ya mchujo shule
sita bora zitaingia fainali na kushindana kupata shule tatu bora.
Katika mashindano haya washindi
watapata zawadi ya pesa taslimu kuanzia shilingi laki mbili hadi elfu
hamsini ambazo zinatolewa na TRA na Benki ya NMB kwa uande wao watatoa
zawadi ya kuwafungulia akauti washindi wa jumla watano pamoja na zawadi
nyingine.
Washindi wapo katika makundi sita
ambayo ni wawasilishaji bora wa mada, washindi wa jumla, walimu bora,
shule bora, mwanafunzi aliye wasilisha mada vizuri, na mchoraji mzuri wa
katuni.
Mashindano haya ambayo
yanaandaliwa na TRA kwa kushurikiana na Songea Mississippi (SOMI) ambao
ni waandaaji wa Tamasha la Serebuka yanafanyika kwa mara ya pili tangu
yaanzishwe Mwaka 2017 mkoani Ruvuma ambapo shule za sekondari hufanya
mdahalo kuhusu mada yoyote ya kodi iliyochgauliwa na washindi hupata
zawadi. Mada inatojadiliwa katika mashindano ya mwaka huu ni ‘Mashine za Kodi za Kielektroniki’
No comments :
Post a Comment