Waziri wa Madini Angellah Kairuki
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji kutoka Shirikisho
la Madini ya Granite la nchini India na wataalam kutoka Wizara ya Madini
na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini
ya Granite na Viwanda vya Mawe la nchini India, Keshava Murthy,
akiweleza jambo Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
(katikati) akiongoza kikao kati ya Wawekezaji kutoka Shirikisho la
Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry).
………………
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry) ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Uongezaji Thamani Madini ya Mawe yenye thamani ya Granite na Mable.
Akizungumza katika kikao
kilichofanyika leo tarehe 18 Julai, jijini Dar es Salaam, Waziri Kairuki
ameueleza ujumbe huo kuhusu adhma ya Tanzania kukakaribisha wawekezaji
katika
ujenzi wa vinu vya kuyeyusha madini ya metali, usonara pamoja na
ukataji na ung’arishaji madini ya vito hususan madini ya Tanzanite
ambayo kwa kiasi kikubwa yamekua yakisafirishwa nje ya nchi yakiwa
ghafi.
“ Sheria yetu ya Madini ya
Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017, imekataza usafirishaji wa
Makinikia pamoja na madini ghafi nje, ndiyo maana tunakaribisha
wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini ndani
ya nchi,” amesema Waziri Kairuki.
Pia, Waziri Kairuki
amewashauri wawekezaji hao kukutana na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) ili kuona namna bora ya kushirikiana katika miradi mbalimbali
ikiwemo ya mawe yenye thamani, bati na madini mengine.
Vilevile, Waziri Kairuki
amelitaka shirikisho hilo kuona namna ambavyo linaweza kushirikiana na
wachimbaji wadogo wa madini nchini hususan katika masuala ya masoko na
mitaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Shirikisho la Madini ya Granite na Sekta ya Mawe la nchini India,
Keshava Murthy, amemweleza Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo liko
tayari kuwekeza kwenye madini ya granite pamoja na marble kwa kuanza na
makontena kati ya 20-50 kwa mwezi.
Pia, Murthy ameongeza kuwa,
Shirikisho hilo lina wanachama zaidi ya 1200 ambao wanajihusisha na
shughuli za uongezaji thamani madini ya granite nchini humo.
Kuhusu ushirikiano na STAMICO,
Murthy amemwahidi Waziri Kairuki kuwa, shirikisho hilo litakutana na
shirika hilo kwa lengo la kubadilishana ujuzi ikiwemo kuangalia namna
bora ya kushirikiana katika sekta husika.
Aidha, amemweleza Waziri Kairuki kuhusu maonesho ya mawe yenye thamani yanayojulikana kama STONA FARE ambayo huandaliwa na shirikisho hilo na kuongeza kuwa, ni miongoni mwa maonesho makubwa duniani.
Mbali na kukutana na Waziri
Kairuki, wawekezaji hao wanatarajia kuendelea na ziara jijiji Dodoma
ambapo wanatarajia kukutana na na Shirikisho la Wachimbaji wa Madini
Tanzania, kutembelea Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania
(GST) pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye uchimbaji wa Granite
jijini Dodoma.
Kabla ya kuja nchini,
wawekezaji hao walitembelea nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi kwa
lengo la kutafuta fursa za uwekezaji kwenye madini hayo.
Kikao hicho pia, kimehudhuriwa
na Mwakilishi kutoka Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TIC), Wataalam
kutoka Wizara ya Madini wakiongozwa na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini
Kanda ya Mashariki Mhandisi Ally Maganga aliyemuwakilisha Kamishna wa
Madini.
No comments :
Post a Comment