Thursday, July 19, 2018

Bodi yataka Watanzania wengi wajenge SGR

Picha
BODI ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imewataka wasimamizi wa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, kuhakikisha inachukua vijana wengi zaidi wa kitanzania ili wajifunze na kupata uzoefu wa ujenzi wa miradi hiyo kwa faida ya Watanzania wote.

Mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema aliyasema hayo juzi wakati wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambao hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 20. Alisema:
“Tumefurahi kuona kwamba Watanzania wanashiriki ingawa tungependa washirikishwe zaidi, hivyo kwa awamu zijazo tunaamini watashirikishwa zaidi katika ngazi zote, ikiwemo wahandisi mpaka ngazi za wafanyakazi wa kawaida na tunataka vijana ndio waingie kwa wingi ili wajifunze uzoefu kwa ajili ya kutekeleza miradi ijayo”.
“Mradi huu ni mkubwa sana na kwa nchi kama ya kwetu unatokea mara moja katika miaka 100… tumeona Watanzania wanashiriki katika mradi huu kwa asilimia 90 ya wafanyakazi zaidi ya 4,000 wanaofanya kazi katika mradi huu. Tumezungumza na wakandarasi hawa pamoja na wasimamizi wa mradi huu ili vijana wetu waweze kushirikishwa zaidi” amesema.
Profesa Lema alisema reli hiyo itakapokamilika ni muhimu katika usafirishaji ingawa usafirishaji unategemea uzalishaji na kuwataka watanzania wote katika ukanda unapopita reli hiyo kujipanga vizuri na kuzalisha kwa wingi katika kilimo na viwanda ili kuweza kutumia kikamilifu fursa za reli hiyo.
Kwa upade wake, Kaimu Msajili wa ERB, Patrick Balozi alisema mradi huo umeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa vifaa vingi vinavyotumika vinatoka nchini hivyo ni faida kubwa kwa maendeleo makubwa ya uchumi wa viwanda.
Mapema Meneja Msaidizi wa mradi kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora, Chedi Masambaji alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni za kawaida za kiufundi, ikiwemo maji ya chini ya ardhi kuwa juu katika maeneo mengine.
Alisema mradi huo ambao ulianza utekelezaji wake wa awamu ya kwanza Mei, mwaka jana, unapaswa kukamilika Novemba mwakani na kwa sasa mkandarasi ana timu mbili kubwa, ikiwemo kuanzia Dar es Salaam kilomita 0 mpaka kwenye bonde la mto Ruvu ambapo ni kilomita 80.
“Timu ya pili ni kilomita 80 hadi kilomita 202 Morogoro na kazi kubwa kwa upande wa Dar es Salaam ni ujenzi wa daraja kubwa la kilomita 2.5 la kupishana watu na bahari ili kuhakikisha hakuna mwingiliano kati ya treni na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri,” alisema.
Alisema kuanzia Buguruni maeneo yote ya ujenzi yameshasafishwa mpaka Ukonga Majumba Sita na kinachoendelea kwa sasa ni upande wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) kufidia nyumba zilizopo kwa kuwa reli hiyo inapita sehemu yenye makazi ya watu.
Alisema, baada ya wiki mbili au tatu kambi ya Soga wataanza kutengeneza mataruma ya zege na wanategemea baada ya miezi miwili reli zitaanza kuingia nchini ingawa uzalishaji wa reli umeshaanza na baadhi ya wahandisi kwa sasa wapo Japan kwa ajili ya kushuhudia reli na kufanya majaribio kama mkataba unavyotaka.
“Tunategemea kwenye mwezi wa tisa katikati reli zitaanza kuingia na utandikaji wa reli utaanza kufanyika…baada ya mwezi mmoja tunatarajia tutakuwa tumeongeza idadi ya wafanyakazi hadi zaidi ya 5,000 ili kuongeza kasi ya Utekelezaji wa mradi,” alisema.
Alisema, lengo lao ni kuhakikisha ujenzi wa tuta hadi mwisho wa mwaka uwe umekamilika na hadi mwezi wa tano madaraja yawe yamekamilika na kuendelea na ujenzi wa mifumo ya mawasiliano ya umeme.
Alisema kwa makisio ya awali mradi huo una madaraja 75, makalvati 300 na utakuwa na kilomita 205 pamoja na njia za kupishana kilomita 95 na kufanya kuwa na jumla ya kilomita 300 Dar es Salaam hadi Morogoro.
Meneja Mradi Msaidizi wa kipande cha Dar es Salaam Morogoro wa TRC, Machibya Masanja alisema katika kambi ya Soga watazalisha mataruma takribani 500,100 pamoja na madaraja na kwamba mradi huo utakuwa na stesheni kuu sita na utakuwa na mfumo utakaoingiza treni nyingi kwa wakati mmoja.
Akizungumzia suala la umeme alisema wataalamu wamekaa na kuliangalia suala hilo, hivyo treni hizo zitaendeshwa bila kukwama na kusema wanaangalia njia za kuharakisha mradi ili utekelezwe kwa haraka.
Hata hivyo, alisema mradi huo kwa sasa unatekelezwa kwa shifti tatu kila baada ya saa nane hivyo unatekelezwa kwa saa 24 ili kupunguza muda wa utekelezaji wa mradi huo.

No comments :

Post a Comment