Kamishna wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harod Nsekela akizungumza na
waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Taasisi hiyo jengo la Sukari
ghorofa ya Tatu jijini Dar es salaam , kuhusu Kazi ya uhakiki wa mali na
madeni ya viongozi kazi ambayo itajumuisha kuwafuata viongozi kwenye
maeneo yao kuanzia tarehe 18/6/2018 hivyo kila kiongozi baada ya kupewa
barua ya mali zake atatakiwa kujiandaa kuhakikiwa.
Kamishna wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harod Nsekela akisoma moja ya
kifungu kinachotumika kuhakiki mali za viongozi mbele ya waandishi wa
habari leo.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harod Nsekela akimsikiliza Afisa
Habari wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither
Barongo alipokuwa akimkaribisha ili kuzungumza na waandishi wa habari
leo.
Kamishna wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harod Nsekela akiwa katika
picha ya pamoja na John Kaole Katibu Viongozi wa Utumishi wa Umma
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushoto na Waziri Kipacha
Katibu Viongozi wa Siasa Sekretarieti ya maadili Viongozi wa Umma.
Baadhi ya viongozi wa Sekretarieti hiyo na waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
………………………………………………………………………………..
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ni Idara ya Serikali inayojitegema ambayo imeanzishwa
kwa Mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 kusimamia mienendo na tabia za Viongozi wa Umma ili
kuhakikisha kuwa Viongozi hao wanazingatia Masharti ya Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma Sura ya 398 ya Sheria za
Nchi.
Mojawapo ya kazi za Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kupokea Matamko ya Rasilimali na
Madeni ya Viongozi wa Umma na Kuhakiki Mali zilizotajwa kwenye matamko
hayo. Mamlaka hayo yametolewa na Vifungu 18 (2) (a) na 18 (2)
(e)mtawalia vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Sheria
ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 4 ya mwaka 2016.
Mtakumbuka kuwa tarehe 27/12/2017
tulikutana na kuwaeleza kuhusu urejeshaji wa Fomu za Tamko la
Rasilimali na Madeni.Zoezi hilo lilifanikiwa kwa 98% ambapo viongozi
waliotakiwa kurejesha fomu walikuwa 16,339.
Kama nilivyotangulia kuwaeleza
baada ya urejeshaji kukamilika uchambuzi ulifanywa na kuchagua
viongozi946 ambao mali zao zitafanyiwa uhakiki. Lengo la Uhakiki huo ni
kuthibitisha uhalisia wa mali hizo kulinganisha na
Tamko la Rasilimali na Madeni la
Kiongozi, thamani halisi ya mali hizo na uhalali wa mali hizo kwa
kuangalia namna mali hizo zilivyopatikana.
Zoezi la Uhakiki litafanywa na
Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili. Kila Kiongozi anayetakiwa
kuhakikiwa ataandikiwa barua kwanza, ili aweze kujua rasilimali na
madeni yake ambayo yatahakikiwa;Pili waandae nyaraka mbalimbali za mali
hizo na tatu ili waweze kuwaonyesha Maafisa wa Sekretarieti mali hizo
zilipo ili uthamini wa mali hizo uweze kufanyika. Kazi ya uhakiki
itajumuisha kuwafuata viongozi kwenye maeneo yao kuanzia tarehe
18/6/2018 hivyo kila kiongozi baada ya kupewabarua ya kuhakikiwa mali
zake atatakiwa kujiandaa.
Lengo la barua hiyo pia ni
kuepusha watu wenye nia ovu kutumia uwepo wa zoezi la Uhakiki kutapeli
viongozi kwa kuwatisha ili kujipatia manufaa mbalimbali ya
kiuchumi.Viongozi watakaohusika na zoezi la kuhakikiwa wawatake maafisa
wa Sekretarieti kuwaonyesha vitambulisho vyao. Pia Kiongozi ambaye
hataridhika na utambulisho huo anaweza kuwasiliana na Ofisi ya
Sekretarieti ya Maadili kupitia Simu Na. 0222111810/11
Napenda kupitia kwenu kuwapa
taarifa hii viongozi husika na wananchi kwa ujumla kuhusu kufanyika kwa
uhakiki wa Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma. Mahsusi kwa
viongozi ambao hawakuwasilisha nyaraka wanatakiwa kufanya hivyo wakati
wa uhakiki. Nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa ni Hati za Mikopo naHati
za Miamala ya Benki ili kuthibitisha fedha zilizopo Benki na taasisi
mbalimbali za Fedha;
Kwa muhtasari nyaraka kwa kila rasilimali au madeni zinazotakiwa kuwasilisha ni kama ifuatavyo:-
RASILIMALI/MADENI | NYARAKA INAYOTAKIWA | |
Ø Fedha zilizopo Benki / Taasisi nyingine za fedha. | · Nyaraka zinazothibitisha taarifa za mikopo uliyochukua benki
· “Bank Statement”. |
|
Ø Hisa na gawio ndani na nje ya Tanzania. | · Hati ya umiliki wa hisa (Share certificate) idadi na thamani yake.
|
|
Ø Nyumba na majengo mengine ndani na nje ya tanzania. | · Hati miliki/ Nyaraka za umiliki wa Viwanja,
· Hati Miliki/ Nyaraka za umiliki wa Nyumba, · Mkataba wa Mauziano. |
|
Ø Mashamba, mifugo, madini ndani na nje ya Tanzania. | · Nyaraka za umiliki wa Ardhi mfano Hati Miliki, wa mauziano/ kukodi Ardhi n.k
· Leseni ya utafiti, umiliki na uchimbaji Madini · Leseni na nyaraka za umiliki Kitalu/Vitalu vya Madini. |
|
Ø Mashine, viwanda na mitambo ndani na nje ya nchi. | · Leseni ya biashara, cheti cha umiliki. | |
Ø Magari na aina nyingine za usafiri, (boti, ndege, ndani na nje Tanzania. | · Hati ya usajili (kadi ya gari). | |
Ø Rasilimali au maslahi mengine ya kibiashara ndani na nje yaTanzania. | · Nyaraka zinazoonyesha umiliki wa kampuni (Memorandum and Articles of Association), Company Profile, Company Registration). | |
Ø Madeni na mikopo unayodai au unayodaiwa. | · Mkataba wa mikopo
· Taarifa ya mkopo · Taarifa ya salio la makato ya mikopo. |
Mwisho napenda kuwashukuru kwa
kuitikia mwito, kufika kwenu kunadhihirisha umakini wenu katika
kuisaidia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutekeleza
majukumu yake. Kwa dhati napenda kuwashukuru kwa kutumia kalamu na
Sauti zenu kuelimisha viongozi na jamii ya watanzania kuzingatia maadili
katika kujenga uzalendo nchini.
Maadili ni Nidhamu, Nidhamu inajenga Uwajibijkaji, Utu na Haki Kuelekea Uchumi wa Kati wa Viwanda.
Jaji (Mst.) Harold R. Nsekela
KAMISHNA WA MAADILI
No comments :
Post a Comment