HESLB
YATANGAZA KUANZA KUPOKEA MAOMBI YA MIKOPO KWA MIEZI MWILI
·
TZS 427 bilioni zatengwa
·
Wanafunzi wapya zaidi ya 40,000 kunufaika
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
leo imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa muda wa
miezi miwili na kusisitiza kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema leo
(Alhamisi, Mei 10, 2018) jijini Dar es salaam fungua rasmi kuwa
mtandao wa kuwasilisha maombi (www.olas.heslb.go.tz)
utakuwa wazi kuanzia leo, Mei 10, 2018 hadi Julai 15, 2018 ili kuwapa fursa wanafunzi
wahitaji kuwasilisha maombi yao.
“Mwaka jana tulitoa mwezi mmoja, mwaka huu tumetoa
muda zaidi ili kuwawezesha kusoma mwongozo kwa makini na kuzingatia maelekezo
tunayoyatoa,” amesema Bw. Badru katika mkutano na wanahabari ambapo pia
alizungumzia mambo muhimu yaliyomo kwenye mwongozo unaojumuisha sifa na
taratibu za utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019. Mwongozo huo unapatikana katika
lugha za Kiswahili na Kiingereza kwenye tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz)
Mambo muhimu yaliyomo
kwenye Mwongozo
Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa katika utoaji
mikopo kwa mwaka 2018/2019, kipaumbele kitatolewa kwa watanzania wahitaji wanaosoma
kozi zenye uhitaji mkubwa zaidi kitaifa kama walimu wa masomo ya sayansi na hisabati;
na sayansi ya afya ya binadamu.
“Tutatoa kipaumbele pia kwa waombaji mikopo watakaodahiliwa
katika kozi zinazohitajika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi
wa aina zote; kozi za sayansi za kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi
na nishati,” amesema Bw. Badru katika mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi
wa wadau wa HESLB kama Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu
ya Juu (TAHLISO); Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Shirika la
Posta (TPC).
Aidha, ameongeza kuwa watanzania wahitaji ambao ni
yatima na wana nakala za vyeti vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa
Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) nao watapewa kipaumbele bila kujali kozi
wanazosoma. Wengine watakaopewa kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu
uliothibitishwa na Mganga wa Mkoa au Wilaya na waombaji mikopo ambao walifadhiliwa
katika masomo yao ya stashahada (diploma) au sekondari na wana barua za
uthibitisho kutoka taasisi zilizowafadhili.
Bajeti na idadi ya
watakaopata mikopo kwa 2018/2019
Kuhusu malengo ya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo
2018/2019, Bw. Badru amesema Bodi imepanga kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi
wapya 40,000 na wanaoendelea zaidi ya 80,000. Kati yao, wanawake watakuwa
asilimia 35 (14,000) na wanaume asilimia 65 (26,000). Bajeti ya fedha za mikopo
kwa mwaka 2018/2019 ni TZs 427 bilioni.
Maboresho yanayoendelea
Kuhusu uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, Bw. Badru
amesema Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Kitengo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu
cha Dar es salaam (UCC) wanaendelea na maboresho makubwa ili kuifanya mifumo ya
utoaji na urejeshaji mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wateja. Kazi hiyo inatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
“Kwa mfano, mfumo wa kuwasilisha maombi sasa
umeboreshwa na kuwa rafiki zaidi kwa kuwa unamwongoza mwombaji katika kila
hatua – na hatoweza kwenda hatua inayofuata kabla ya kukamilisha hatua ya awali,”
amesema Bw. Badru.
Aidha, kwa mara ya kwanza, Bodi imetoa mwongozo wake
wa uombaji mikopo katika lugha ya Kiswahili pamoja na kitabu chenye maswali na
majibu 21 kuhusu sifa na utaratibu (hatua kwa hatua) wa kuwasilisha maombi ya
mikopo. Kitabu na mwongozo vinapatikana katika tovuti ya Bodi na vitasambazwa
kwa wadau kuanzia wiki ijayo ambapo maafisa wa Bodi watatembelea shule na
waombaji nchini kote.
Maoni ya TAHLISO
Akiongea katika mkutano huo, Meneja Usajili wa RITA
Bi. Patricia Mpuya amewahakikishia waombaji wa mikopo kuwa vyeti vya vifo na
kuzaliwa ambavyo vitawasilishwa kwa taasisi hiyo kuwa vitahakikiwa ndani ya
siku tatu.
“Tunawakumbusha kuhakikisha wanaleta maombi haraka
badala ya kusubiri ‘deadline’ (muda
wa mwisho) na sisi tumejipanga wanapata majibu ya uhakiki ndani ya siku tatu
tangu tuyapokee,” amesema Bi. Mpuya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shirika Posta (TPC) Bw.
Hassan Mwangombe, ambao watapokea na kusafirisha kwenda HESLB fomu za maombi ya
mikopo, amesema wamejipanga kutoa huduma za elimu kwa waombaji na intaneti
katika vituo vyao zaidi ya 180 nchini. Aidha, wameandaa bahasha maalum ambayo
mwombaji mkopo atajaza taarifa zake muhimu ili kurahisisha uwasilishaji wa
maombi hayo kwa HESLB.
Mwenyekiti wa TAHLISO Bw. George Mnali amezitaka
RITA na TPC kuhakikisha wanatekeleza mipango yao ya kuwahudumia waombaji mikopo
kama walivyoahidi na kuongeza TAHLISO itatumia muda wa miezi miwili
kuwaelimisha wanafunzi wasio na mikopo lakini wana sifa kuomba na kufuata
maelekezo ya Bodi.
Wito
Bodi imewataka waombaji mikopo kuzingatia maelekezo
yaliyotolewa na wale ambao wana uwezo wa kugharamia elimu ya juu kutoomba mkopo
ili kutoa fursa kwa wahitaji halisi wengi zaidi kuomba na kupata mikopo.
HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine,
kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na kukusanya
mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.
Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Alhamisi, Mei 10, 201
No comments :
Post a Comment