Baadhi ya waalikwa katika shughuli
ya ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya ABC Jijini Dodoma
lililofunguliwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dkt. Bilinith Mahenge, wakizungumza jambo kabla ya kufungua rasmi tawi
la Benki ya ABC Jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa tawi la Benki
ya ABC Bw. Imani John, akieleza kuhusu lengo la kufungua rasmi tawi
jipya la Benki hiyo Jijini Dodoma kuwa ni kuleta karibu huduma za
kibenki kwa wananchi wa Jiji hilo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony
Mavunde, akiishukuru Benki ya ABC kwa kuleta huduma za kibenki karibu na
wananchi wa Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt.
Bilinith Mahenge, akiwataka wananchi wa Jiji la Dodoma kutumia fursa za
huduma za kifedha zilizopo katika Jiji hilo ili kujiendeleza kiuchumi,
wakati wa kufungua rasmi tawi jipya la Benki ya ABC Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto) akifungua rasmi tawi la Benki
ya ABC Jijini Dodoma, kushoto ni Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde na
wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kulia), akikata utepe kuashilia
kufunguliwa rasmi kwa tawi jipya la Benki ya ABC Jijini Dodoma huku
akishuhudiwa na Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde (kushoto), Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge (kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Benki
hiyo Bw. Imani John, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja
na viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa Benki ya ABC baada ya
kufunguliwa rasmi kwa tawi jipya la Benki hiyo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya wananchi na wageni waalikwa baada ya kufunguliwa rasmi kwa
tawi jipya la Benki hiyo Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango
……………….
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI imelipa madeni ya
wakandarasi na watoa huduma mbalimbali yanayofikia zaidi ya
shilingi
trilioni 1.2 katika mwaka huu wa fedha hatua iliyochangia kuongeza
ukwasi wa fedha katika jamii ikiwa ni hatua ya Serikali ya kuhakikisha
kuwa uchumi wa nchi unakua kwa haraka.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma, na
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akifungua
rasmi tawi la benki ya ABC, lililoanzisha huduma zake za kibenki mkoani
humo tangu Januari mwaka huu.
Alisema kuwa hatua hiyo
imechukuliwa ili kuwaongezea uwezo wajasiriamali na wafanyabiashara
waliotoa huduma Serikalini ili waongeze mzunguko wa fedha katika uchumi.
Ametoa rai kwa wakazi wa mkoa wa
Dodoma kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Benki hiyo ambayo
riba yake haizidi asilimia 17 ili waweze kuendeleza shughuli za
uzalishaji mali na huduma za jamii kwa kuwekeza katika miradi
inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
“Ni matarajio yangu kuwa sehemu
kubwa ya mikopo itakayotolewa na Benki yetu ya ABC, itaelekezwa kwenye
sekta ya kilimo na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, vya kati, mifugo,
uvuvi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na misitu” alisema Dkt.
Kijaji
Dkt. Kijaji alisisitiza umuhimu wa
uwepo wa sekta imara ya fedha itakayochochea ujenzi wa viwanda
vitakavyo saidia kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo pamoja na kukuza
ajira kwa vijana.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki
hiyo ya ABC Bw. Imani John, alieleza kuwa Benki yake yenye mtaji wa
zaidi ya shilingi bilioni 67 imeendelea na jitihada zake za kupanua
huduma zake ili kukidhi mahitaji ya kibenki ya wananchi.
Alisema kuwa benki yake imeanzisha
huduma zake katika Jiji la Dodoma kufuatia utafiti uliofanyika hivi
karibuni unaoonesha kuwa asilimia 13 pekee ya wakazi wa mkoa huo
wanafikiwa na huduma za kipenki, pamoja na uamuzi wa benki hiyo wa
kuunga mkono hatua ya Serikali ya kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa Makao
Makuu ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Mhe. Anthony
Mavunde, ameishukuru Benki ya ABC kwa kupeleka huduma za kibenki karibu
na wananchi wa Jiji la Dodoma na kuwataka wananchi wa mkoa huo
kuchangamkia fursa za mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kujiletea
maendeleo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.
Binilith Mahenge, pamoja na kuipongeza Benki ya ABC kwa hatua yake ya
kusogeza huduma za kibenki kwa wakazi wa Jiji la Dodoma, amezitaka
taasisi nyingine kuwekeza katika sekta hiyo pamoja na huduma nyingine
kama vile ujenzi wa Hoteli za kisasa kwa kuwa mkoa huo una fursa nyingi
ikiwemo ardhi yenye rutuba.
Benki ya ABC inafanya huduma zake
hapa nchini kwa zaidi ya miaka 20 na inamilikiwa na wanahisa akiwemo
TDFC ambaye ni mbia wa ABC Holding Ltd, anayemiliki asilimia 14.7, kati
ya asilimia hizo 14.7, asilimia 68 zinamilikiwa na ABC Holding ltd, na
asilimia 32 zinamilikiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina.
No comments :
Post a Comment