Na Lydia Churi, Magreth Kinabo-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amesema Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) ni
taasisi ya Umma na siyo binafsi hivyo amekitaka kutekeleza majukumu yake
ya msingi ya kisheria kwa kushirikiana na Mahakama na kuacha kujiingiza
kwenye
masuala ya uanaharakati na siasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
leo jijini Dar es salaam Jaji Mkuu amesema TLS ni chama huru cha
kitaaluma kwa kuwa kilianzishwa kwa mujibu wa sheria kufanya kazi kwa
manufaa mapana ya Umma.
“Hatuwezi kukubali chama hiki
kikajisemea kuwa wao ni chama binafsi na tukakubali, dhana ya ubinafsi
haipo”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema jukumu la TLS ni Kuisaidia
Serikali na Mahakama kuhusu mambo yoyote yanayogusa sheria, utawala wa
sheria na kazi za kisheria na akaongeza kuwa dhana hii ndiyo
inayoiunganisha Taasisi hiyo na Mahakama ya Tanzania.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka
viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama pamoja na Mihimili mingine ya
dola na kuacha malumbano kwenye vyombo vya habari kwa kuwa hayawasaidii
kuendeleza chama hiki muhimu kwa wanasheria nchini.
Jaji Mkuu pia amewashauri viongozi
wa chama hicho kumuheshimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa Sheria
na Kanuni zote ni lazima zipitie kwake.
Alisema Mamlaka ya Baraza la
Uongozi la TLS katika Kutekeleza Majukumu ya Umma ni kusaidia kuboresha
elimu ya sheria na taaluma ya Sheria Tanzania na kuwawezesha wanataaluma
wa sheria kupata elimu ya ziada ya sheria kwa kadri mabadiliko
yanayotokea nchini na duniani.
Majukumu mengine ya TLS ni
pamoja na kuwawakilisha, kuwatetea na kuwasaidia wanasheria Tanzania
kuhusu mazingira ya kufanya kazi za kisheria na kuwasaidia wananchi wa
Tanzania katika masuala ya kisheria yanayogusa Sheria.
TLS ni Taasisi iliyoanzishwa
kwa mujibu wa Sheria za nchi kabla ya Uhuru na kukubalika kuendelea
kuwepo kama Taasisi ya Kisheria kwa malengo ya kuanzishwa kwake
kuelekezwa kwenye manufaa ya umma kwa kushirikiana na Mahakama, Bunge,
pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Chama hiki kilianzishwa kwa
Sheria ya Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) Namba 30 ya
1954 na ni moja ya Sheria nyingi za iliyokuwa Tanganyika kabla ya Uhuru,
ambazo kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Katiba ya Tanganyika
ziliruhusiwa kuendelea kutumika Tanganyika ilipopata Uhuru Disemba 9
mwaka 1961 kama Sheria za Tanganyika huru.
No comments :
Post a Comment