Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH). Prof. Lawrence Museru akiongoza kikao cha
Baraza la Wafanyakazi la hospitali hiyo jana. Kushoto ni Katibu Msaidizi
wa baraza hilo, Merina Rwechungura na kulia ni Katibu wa Baraza hilo,
Elineza Msuya.
Wajumbe wakipitia makabrasha kwenye mkutano huo.
Mwakilishi wafanyakazi wa hospitali hiyo, Judith Nyaruga akichangia mada kwenye mkutano huo jana.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wawakilishi wa wafanyakazi.
Mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Deus Buma akichangia mada kwenye mkutano huo.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
…………….
Wafanyakazi
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwamo madaktari na wauguzi
wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kwamba
atakayekwenda kinyume na agizo hilo atachukuliwa hatua na mamlaka
husika.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Lawrence
Museru kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi ambako kulijadiliwa mambo
mbalimbali yakiwamo
huduma bora kwa wagonjwa, mafanikio, maslahi kwa
wafanyakazi na mikakati ya kujenga miundombinu mipya na kukarabati ile
ya zamani.
Katika
mkutano huo Prof. Museru amewataka wafanyakazi kutoa taarifa za
watumishi wenzao wanaotoa huduma zisizoridhisha kwa wagonjwa pamoja na
wateja wengine wanaofika MNH kwa ajili ya kupatiwa huduma.
“Watumishi
watakaotajwa kwamba wanatoa huduma mbaya kwa wagonjwa na wateja wengine
watachukuliwa hatua, lengo ni kuboresha huduma za afya,” amesema Prof.
Museru.
Prof.
Museru amewasisitiza wafanyakazi kutoa ushirikiano katika mikakati
inayoendelea ya kutoa huduma bora za kibingwa ikiwamo upandikizaji wa
figo, upandikizaji wa vifaa vya usikivu kwa watoto wasiosikia na huduma
mbalimbali za kibingwa.
Mkurugenzi
huyo amewaeleza wafanyakazi kwamba hospitali inaendelea kutoa huduma
bora za kibingwa ikiwamo upandikizaji wa figo na vifaa vya usikivu kwa
watoto.
Amesema
hospitali ilifanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa mmoja na changamoto
zilizojitokeza tayari zimefanyiwa kazi na hivyo kuwezesha wagonjwa wanne
kupandikizwa figo mwezi huu na kwamba kila mwezi wagonjwa watano
watakuwa wakipandikizwa figo.
“Hospitali
inaendelea kuboresha miundombinu inayotumika wakati wa upasuaji wa
kupandikiza figo na baada ya maboresho haya kila siku mgonjwa mmoja
atakuwa akipandikizwa figo.
Katika
hatua nyingine, Prof. Museru amesema huduma ya upandikizaji vifaa vya
usikivu inaendelea vizuri na kwamba mwishoni mwa mwezi wa tano au wa
sita mwanzoni wagonjwa watano watapandikizwa vifaa vya usikivu na kwa
mwaka wagonjwa 24 watakuwa wamepatiwa huduma hiyo.
Amesema
pia hospitali ipo kwenye mikakati ya kujenga jengo jipya ambalo
litatumika kulaza wagonjwa na kutoa huduma mbalimbali ikiwamo
upandikizaji wa figo.
Naye
Mkurugenzi wa Fedha wa Hospitali hiyo, Gerald Jeremiah amewataka
wafanyakazi hao kujenga tabia ya kufuatilia michango yao sehemu husika
ili kuweka taarifa vizuri ya mafao yao kabla ya kustaafu.
No comments :
Post a Comment