Na. Immaculate Makilika
Mapema wiki hii, tumeshuhudia Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akihutubia
kikao cha Bunge la Afrika Mashariki kilichofanyika mjini Dodoma, akiomba
Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kutumia lugha adhimu ya Kiswahili
wakati wa
uendeshaji wa vikao vyao katika kuenzi lugha hiyo kongwe na
maarufu ikikadiriwa kuwa ni tangu katika milenia ya kwanza tangu
kuzaliwa kwa Yesu Kristo, yaani mnamo miaka ya 800 hadi 1000.
Ambapo Rais Magufuli anasema
“nimefurahi kusikia Spika wa Bunge hili amesoma Tanzania, sekondari hadi
chuo kikuu na baada ya kumaliza hapa, ndipo akarudi nchini mwao Rwanda
na nimefurahi kusikia Kiswahili kitaendelezwa katika bunge hili”.
Huku akiunga mkono kauli ya Spika
wa Bunge hilo Dkt. Martin Ngoga kuwa wanahitaji kuendeleza matumizi ya
Kiswahili katika Bunge lao.
Ambapo kukipa hadhi zaidi
Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki, Jumuiya hiyo ilianzisha
Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ikiwa ni sehemu ya ufufuzi
wa Kamati ya Taifa ya Lugha iliyoanzishwa na Wakoloni 1930 ili
kuendeleza matumizi ya Kiswahili.
Tukumbuke kuwa lugha hii ya
Kiswahili ambayo imekuwa ikizungumzwa nchini Tanganyika na Zanzibar
tangu enzi za ukoloni, ilikuwa chachu ya kuchagiza nchi hizi mbili
kuungana mnamo April 26, 1964.
Leo tunapoadhimisha miaka 54 ya
Muungano wa Taifa la Tanzania, Kiswahili kimewakusanya na kuwajumuisha
pamoja watu wa makabila zaidi ya 120 kikitumika kuwa lugha ya
mawasiliano inayoeleweka na watu wote. Hii si ajabu, ikizingatiwa kuwa,
kwa asili yake, Kiswahili ni lugha unganishi, yaani yenye hulka ya
kuunganisha na siyo kutenganisha au ya kibaguzi (Mazrui & Mazrui
1999) kama, kwa mfano, Kiafrikana.
Mazrui anayasema hayo katika kitabu maarufu cha Political Culture of Language: Swahili, Society and the State.
Ama kwa hakika Kiswahili kinavuka
mipaka si tu imekuwa na sifa kuu ya kuunganisha watanzania, waafrika
mashariki ila lugha hii adhimu imeendelea kusaambaa duniani kote.
Aidha Kiswahili kinatambulika kuwa
lugha ya kazi katika Jumuiya za Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika,
ambapo kwa kuzingatia hilo, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano
alithibitisha hili alipohutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za
Umoja wa Afrika kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza alipokuwa akiaga AU
Julai , 2004 Addis Ababa, Ethiopia.
Waasisi wetu yaani Hayati Mwalimu
Julius Nyerere pamoja na Hayati Abeid Aman Karume, walifanya mengi kwa
kutumia lugha hii adhimu ya Kiswahili. Na kwa kutumia lugha hii adhimu
wameweza kujenga umoja wa kitaifa na utamaduni wa kiafrika pamoja na
kuushinda ubaguzi wa rangi, kutetea usalama wa Taifa katika vita dhidi
ya Nduli Idi Amin Dada wa Uganda.
Leo tunapoadhimisha miaka hii 54
ya Muungano wetu mujarabu tunayo mengi ya kujivunia kwa hatua muhimu tu
tunazoendelea kupitia, ambapo Kiswahili kimekuwa ni moja ya nyenzo
muhimu.
Kiswahili kimekuwa mithili ya
mhisopo (mmea wenye harufu nzuri), kama ambavyo tunashuhudia Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea
kukienzi, kukikuza, kukieneza na kukipa heshima zaidi kwa kukitumia
kikiwa lugha yake rasmi katika shughuli za kitaifa na kimataifa.
Mfano, Rais Magufuli amehutubia
Kikao cha 17 cha Dharura cha Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika
Mashariki (EAC) kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa kutumia lugha
adhimu ya Kiswahili. Januari 29 mwaka 2017 Rais Magufuli amehudhuria
mkutano wa 28 wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Mjini Addis Ababa,
Ethiopia na kuhutubia kwa lugha aushi ya Kiswahili.
Halikadhalika, amehutubia kwa
lugha ya Kiswahili katika ziara mbalimbali za viongozi wa Kimataifa hapa
nchini kama ile ya Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliyefanya ziara
yake nchini Julai 11 mwaka 2016. Aidha, Katika azma hii Rais Magufuli
amesisitiza kuwa “lengo la kutumia lugha hiyo ni kukikuza na kukitangaza
Kiswahili kama lugha mama ya taifa.”
Huu ni muda muafaka Watanzania
wanapotakiwa kukitazama Kiswahili zaidi ya sasa, nikimaanisha kwamba
huenda katika mwaka 2064 yaani katika maadhimisho ya miaka 100 ya
Muungano kutakuwepo na watu wengi wa aina ya Rais Magufuli ambao
hawataona soni kuzungumza lugha hii adhimu katika mikutano mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Kwa kuangalia namna ambavyo lugha
hii imeendelea kushika hatamu, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)
limeandaa mpango wa kuhakikisha lugha hiyo adhimu inakuwa bidhaa ya
kimataifa na itakayounganisha watu wengi zaidi duniani ikiwa ni pamoja
na kutoa ajira kwa wapenzi na wadau wake.
Baraza limeweka mikakati
ya kuchangamkia fursa zinazojitokeza za walimu wa Kiswahili katika nchi
za nje ambapo Serikali kupitia BAKITA itaandaa mpango ambao utawezesha
taifa kunufaika na utaalamu wa walimu hao kwa kiasi fulani cha mapato
yao kurejeshwa katika mfuko wa taifa.
Katibu Mtendaji wa Bazara la
Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dkt. Selemani Sewanga anasema katika
mahojiano maalum kuwa watanzania ni lazima wajivunie lugha hii adhimu
kwa kuwa imeendelea kukua kwa kasi duniani na kuifanya kuwa si lugha ya
Tanzania pekee, bali Afrika Mashariki lakini pia ni lugha ya 10 kwa kuwa
na wazungumzaji wengi zaidi duniani ambapo inakadiriwa kuzungumzwa na
watu takribani milioni 200 duniani kote.
Kutokana na umuhimu wa lugha hii,
baadhi ya wageni mbalimbali wanaokuja nchini kwa ajili ya utalii au
kufanya kazi wamekuwa wakifanya jitihada kujifunza Kiswahili.
“Ni lugha inayoendelea kukua kwa
sababu ya asili yake na kumekuwepo shughuli za ukuaji wa uchumi ikiwemo
uchimbaji gesi na madini mbalimbali, shughuli hizi zinasaidia wageni
kujifunza lugha hii adhimu ili waweze kuwasiliana na wenyeji,” anasema
Dkt. Sewange.
Hivi sasa kuna nchi mbalimbali
duniani zimeanzisha programu ya somo la Kiswahili katika vyuo vyake
vikuu au katika taasisi zake za lugha ya kigeni. Baadhi ya nchi hizo ni
pamoja na Marekani, Uchina, Urusi, Italia, Ujerumani, Korea Kusini, na
ufaransa.
Aidha, Kiswahili kinatumika katika
idhaa mbalimbali za kimataifa kama vile Sauti ya Amerika, Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC), Redio Deusche Welle, Redio France
International, China Redio International, Idhaa ya Kiswahili Redio
Japan, Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran, Idhaa ya Kiswahili Redio ya
Umoja wa Mataifa, Redio Vatican, Redio India, Redio ya Korea Kusini na
Redio Moscow International.
Kiswahili sasa kitafundishwa kama
chanzo cha ajira tofauti na mtazamo uliokuwepo zamani. Hivi sasa
wataalamu wa Kiswahili wanaandaliwa kwa kulenga soko mfano wanafundishwa
tafsiri na ukalimani ili waweze kwenda kutoa huduma hiyo ndani na nje
ya nchi.
Kushamiri huku kwa matumizi ya
Kiswahili duniani kunategemea zaidi mipango madhubuti ambayo Serikali
imeendelea kuweka kwa ustawi wake ikiwa pamoja na kuwa na kanzidata ya
wataalamu wa Kiswahili nakupata taarifa sahihi za wataalamu wote nchini
ili ile rahisi kuwasiliana nao pale zinapotokea fursa za ndani na nje ya
nchi.
Licha ya kuwa Kiswahili ni lugha
ya pili kwa kuwa na wazungumzaji wengi barani Afrika, juhudi zaidi
zinahitajika kuikuza zaidi lugha hii. Katika kuadhimisha miaka 54 ya
Muungano, huu ni wakati muafaka sasa wa kuhakikisha Kiswahili si tu
kinaunganisha watanzania na waafrika lakini pia kiwe chachu ya maendeleo
na kuitambulisha Tanzania kimataifa.
No comments :
Post a Comment