Muuguzi Neema Mlay akitoa chanjo
ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa mwanafunzi Happiness Robert wa Shule
ya Sekondari Simiyu wakati wa Uzinduzi wa chanjo hiyo Mkoa wa Simiyu
katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini Bariadi, (kulia)
Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka akishuhudia zoezi hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,
Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa baadhi ya Shule za Msingi
na Sekondari za Mjini Bariadi wakati wa uzinduzi wa Utoaji wa chanjo ya
Saratani ya mlango wa Kizazi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na
Sima B Mjini Bariadi.
Flora Masunga mwanafunzi wa Shule
ya Msingi Sima B akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani)
baada ya kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi mara baada ya
uzinduzi wa Utoaji wa chanjo hiyo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A
na Sima B Mjini Bariadi.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Simiyu,
Baetrice Kapufi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
baada ya Uzinduzi wa zoezi la chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi
uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini
Bariadi.
……………………
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka amezindua rasmi leo zoezi la chanjo ya Saratani ya Mlango
wa Kizazi ambayo inatarajiwa kutolewa kwa watoto wa kike takribani
37,141 wenye umri wa miaka 14 kwa mkoa mzima wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika katika
Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B na kushirikisha watoto wenye
umri wa miaka 14 kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na
Sekondari
za Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Akizungumza na wanafunzi
walioshiriki katika uzinduzi wa chanjo hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka
wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kuwahamasisha wenzao kwenda kupata
chanjo na kuwahamasisha wazazi kuwahimiza watoto wa kike wote wenye umri
wa miaka 14 kwenda kupata chanjo hiyo.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Simiyu
Bibi.Beatrice Kapufi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto
wenye umri wa miaka 14, wanapata haki yao ya kupata chanjo ya Saratani
ya Mlango wa Kizazi ambayo itatolewa bila malipo katika vituo vya
kutolea huduma za afya, shule za Msingi na Sekondari.
Aidha, amesema Mkoa kupitia
Kitengo cha Huduma za Chanjo wameshatoa mafunzo kwa watendaji, watoa
huduma wote wa vituo vinavyotoa huduma ya chanjo na walimu
wanaojishughulisha na huduma za Afya katika Shule za Msingi na Sekondari
zote mkoani Simiyu.
“Nitoe wito kwa wazazi wote
kuhakikisha watoto wa kike wote wenye miaka 14 wanapata haki yao msingi
kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi, chanjo hii inatolewa bure
na itatolewa mara mbili, mtoto akishapata kwa mara ya kwanza atatakiwa
kwenda kupata chanjo ya pili baada ya miezi sita” alisema Kapufi.
Nao wanafunzi waliopata chanjo
wameishukuru Serikali kwa kuwaletea chanjo hiyo ambayo wamesema
itawasaidia kujikinga na maambukizi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
“Tunashukuru sana Serikali kwa
kutuletea chanjo hii itatusaidia tusipate Saratani ya Mlango wa Kizazi,
nawaomba wazazi wawaambie wenzetu nao waende wakapate chanjo hiyo, ili
wasipate Saratani wakiwa wakubwa” alisema Flora Masunga mwanafunzi wa
Shule ya Msingi Sima B.
No comments :
Post a Comment