NA WAMJW-DAR ES SALAAM.
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewashauri wananchi
kwenda vituo vya tiba haraka mara baada ya kugundua kuwa wana dalili za
ugonjwa wa dengue.
Hayo ameyasema wakati alipotoa
tamko juu ya kuingia kwa ugonjwa wa dengue hapa nchini mara baada ya
kufunga Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri wa Afya wa Nchi za Afrika
Mashariki, Kati na Kusini ECSA leo jijini Dar es salaam.
“Kuna dalili za Ugonjwa Dengue
zikiwemo homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususan sehemu za macho, maumivu
ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi
14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue hivyo Wizara
inashauri kuwa wananchi wasiwe na hofu, bali mara tu wanapoona dalili za
ugonjwa waende katika vituo vya tiba alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa
Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili
za malaria hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa, wakipata homa wahakikishe
kuwa wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au Dengue, au
sababu nyingine, ili hatua stahiki zichukuliwe.
Waziri Ummy amesema kuwa ili
kujikinga na ugonjwa huo ni lazima Kuangamiza mazalio ya mbu kwa kufukia
madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya
mbu kwenye madimbwi hayo pamoja na Kujikinga na kuumwa na mbu kwa kuvaa
nguo ndefu muda wote hasa nyakati za mchana.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa
Wizara itaendelea Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa
kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa (IDSR), ambapo tunaendelea
kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na Kutoa
elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
Mbali na hayo Waziri Ummy
amesisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya
wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na Wizara itaendelea
kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kufuatilia na kudhibiti
ugonjwa huo.
Homa ya Dengue ni ugonjwa
unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni
weusi wenye madoa madoa meupe yenye kung’aa.
No comments :
Post a Comment