WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa za Afrika kutoa mapendekezo
ya namna ya kutokomeza magonjwa yasiyo ambukiza kwa wakuu wa nchi hizo
ili yafanyiwe kazi.
Aliyasema hayo jana jioni
(Jumatatu, Machi 19, 2018) wakati akifungua Mkutano wa 65 wa
Mawaziri wa
Afya kutoka nchi tisa wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika
Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC)
Alisema magonjwa yasiyo ambukiza
ni miongoni mwa magonjwa ambayo yameendelea kuwatesa wananchi kwa kiasi
kikubwa katika nchi nyingi za Bara la Afrika, hivyo vema mawaziri hao
wakatoa mapendekezo ya namna ya kuyatokomeza.
Waziri Mkuu alisema magonjwa hayo
yanaweza kudhibitiwa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha lishe na
kusisitiza ulaji wa vyakula bora, kufanya mazoezi na kubadili mitindo ya
maisha.
“Magonjwa yasiyoambukiza
yanaongoza kwa kusababisha vifo katika baadhi ya nchi wanachama wa ECSA.
Magonjwa haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo
wetu wa lishe na maisha, hivyo ni muhimu suala hili likatafutiwa
ufumbuzi.”
Waziri Mkuu alisema magonjwa
yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine ya milipuko kama ebola, homa
ya bonde la ufa, dengue, homa ya manjano yamekuwa kikwazo cha maendeleo
kwa katika baadhi ya nchi.
Pia, Waziri Mkuu aliongeza kuwa
sekta ya afya ni muhimu kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya nchi zote
zikiwemo zilizoendelea na zinazoendelea, hivyo changamoto zote
zinazoikabili zinapaswa zipewe kipaumbele katika utatuzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya,
Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu alisema
malengo ya mkutano huo ni kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazohusu
sekta ya Afya na kuyapatia ufumbuzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na
Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za
Afrika Mashariki, Kati na Kusini ambazo ni Tanzania, Malawi, Lethoto,
Uganda, Kenya, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Muwakilishi kutoka nchini
Mauritious.
Pia Katibu wa jumuiya hiyo Profesa
Yoswa Dambisya, Muwakilishi wa Benki ya Dunia Dkt. Paolo Belli pamoja
na wadau wa sekta ya afya kutoka nchi hizo.
No comments :
Post a Comment