Meneja Ofisi ya Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) Zanzibar, Bi. Esuvatie-Aisa Masinga akitoa
taarifa ya hali ya mawasiliano Zanzibar kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) wakati wa
ziara yake kisiwani humo
Meneja Msaidizi Mtandao wa Shirika
la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Zanzibar Bwana Mohamedi Ali Haji
akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta
Nditiye (wa kwanza kushoto) njia yanakopita mawasiliano kutoka Dares
Salaam kuja Zanzibar wakati wa ziara yake kisiwani humo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ( wa kwanza kulia) akisikiliza
kwa makini maelezo kutok akwa mfanyakazi wa TTCL kuhusu mwitikio wa
wateja kwa huduma zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)
wakati wa ziara yake Zanzibar
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano (kulia) akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bwana John Munkondya kuhusu vituo vya
mawasiliano vilivyopo Zanzibar wakati wa ziara yake kisiwani humo
Mfanyakazi wa Shirika la Posta
Tanzania (TPC) Zanzibar, Bwana Khalfan Mmkahirika akimuonesha Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano namna scanner inavyofanya kazi ya
kukagua mizigo na vifurushi vinavyosafirishwa na Shirika hilo ndani na
nje ya nchi ili kulinda usalama wa raia na taifa wakati wa ziara yake
Zanzibar. Mwenye koti nyeusi ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo
Bwana Hassan Mwang’ombe
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa waandishi wa
habari (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwa taasisi za mawasiliano
Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo Bwana
Hassan Mwang’ombe na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma wa Shirika la Simu
Tanzania (TTCL) Bwana Hussein Selemani Nguvu.
……………….
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameupa Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) wiki mbili kwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano ya
simu
za mkononi na kuwasilisha taarifa hiyo ofisini kwake.
Mhandisi Nditiye ameyasema hayo
akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua hali ya
mawasiliano kisiwani humo na kutembelea taasisi za mawasiliano zilizo
chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo suala la
mawasiliano ni la muungano.
Nditiye amesema kuwa amepokea
taarifa kutoka kwa wabunge wa Kisiwa cha Zanzibar kuwa hali ya
mawasiliano kwenye kisiwa hicho sio nzuri na sehemu nyingine hakuna
mawasiliano licha ya kuwa kuna minara ambayo inatoa huduma za
mawasiliano ila kutokana na jiografia ya Pemba ambapo kuna milima na
mabonde hivyo mawasiliano si ya uhakika. “Nawaagiza muende Pemba
mkaainishe maeneo yote ambayo hayana mawasiliano na muwasilishe taarifa
hiyo ofisini kwangu baada ya wiki mbili,” amesema Mhandisi Nditiye.
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie-Aisa Masinga wakati
akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye kuhusu majukumu ya ofisi
yake ya usimamimizi na udhibiti wa mawasiliano na posta, amekiri kuwa
yapo baadhi ya maeneo Pemba na Unguja ambapo hali ya mawasiliano sio
nzuri na hairidhishi.
Ameongeza kuwa Pemba kuna maeneo
ambayo hakuna mtoa huduma na pale ambapo mawasiliano yapo bado ubora wa
huduma sio nzuri. Pia ameyataja maeneo yasiyo na mawasiliano kwa upande
wa Mkoani kuwa ni Kengeja na Chokochoko na kwa upande wa Micheweni ni
Konde na Gando.
Amefafanua kuwa sehemu nyingine za
Pemba mtandao wa Zantel upo lakini ‘coverage yake’ sio nzuri. “Ili
kufanya mawasiliano yawe mazuri kwa Pemba, ni muhimu ‘site’ zikaongezwa
hasa ukizingatia hali ya kijiografia ya kisiwa hicho,” amesema Masinga.
Mawasiliano ya kisiwa cha Pemba hayaridhishi, tunapendekeza Serikali
kupitia UCSAF kuweka minara zile sehemu ambazo hakuna mawasiliano.
Naye mwakilishi wa UCSAF Bwana
John Munkondya amepokea maelekezo ya Mhandisi Nditiye ambapo Mfuko huo
utakwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano na kuwasilisha ripoti
ofisini kwake ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano ya
uhakika. “Sisi kama UCSAF tumechukua taarifa hii ya maeneo ambayo hayana
mawasiliano, tutakwenda Pemba kukagua na maeneo hayo yataingizwa kwenye
utaratibu wa kanda maalumu ili tuweze kufikisha mawasiliano,”amesema
Munkondya.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye amekagua utendaji kazi wa moja ya scanner
mpya ambazo Wizara yake imeipatia Shirika la Posta Tanzania ili ziweze
kutumika kukagua mizigo, vifurushi na vipeto ambavyo vinaingia na
kutoka ndani na nje ya nchi ili kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa
bidhaa na vifaa ambavyo ni hatarishi kwa usalama wa raia na taifa letu.
Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika
la Posta Tanzania Bwana Hassan Mwang’ombe amemweleza Mhandisi Nditiye
kuwa Wizara yake imewapatia scanner nne zenye thamani ya shilingi
milioni 421 ambapo tayari zimefungwa kwenye mikoa mbali mbali ili
ziweze kuwasaidia kupunguza udanganyifu ambao unajitokeza ambapo baadhi
ya wateja wasio waaminifu wamekuwa wakisafirisha baadhi ya vifaa na
bidhaa kama vile madawa ya kulevya kinyume na sheria za nchi.
Pia, Mhandisi Nditiye ametembelea
na kukagua maendeleo ya ujenzi, ufungaji wa samani na uwekaji wa vifaa
vya TEHAMA kwenye moja ya kituo cha mawasiliano kilichojengwa na UCSAF
kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za mawasiliano.
Munkondya amemweleza Mhandisi
Nditiye kuwa UCSAF imejenga vituo kumi vya mawasiliano kwa gharama ya
shilingi milioni 721 na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98 ambapo
vituo sita vipo Unguja na vine vipo Pemba. Ameongeza kuwa UCSAF inaweka
samani, vifaa vya TEHAMA pamoja na kompyuta kumi kwa kila kituo,
kujenga choo na uzio ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano
kwa gharama nafuu.
Naye mjumbe wa Bodi ya TPC Bi.
Khadija Shaban amemuomba Mhandisi Nditiye kuwa vituo hivyo vya
mawasiliano vya Pemba na Unguja visimamiwe na kuendeshwa na TPC ili
viweze kudumu kwa muda mrefu kama ambavyo inafanyika hivyo Tanzania
Bara.
Mhandisi Nditiye akiwa katika
ziara yake kisiwani Unguja, ametembelea na kukagua mitambo ya Shirika la
TTCL, hali ya biashara na namna wanavyowahudumia wateja ambapo ameona
miundombinu ya Shirika hilo inavyosambaza huduma za mawasiliano kutoka
Tanzania Bara kuja kisiwa cha Zanzibar.
Nditiye ameiagiza TTCL kufunga
mitambo ya mawasiliano kwenye meli za maziwa makuu na baharini ili
wananchi wanaposafiri waweze kupata mawasiliano ya uhakika ya simu za
mkononi na huduma za intaneti.
Pia, ameiagiza TCRA kuwasajili
watu wote wanaosafirisha mizigo, vifurushi na vipeto na kuwapatia leseni
ili walipe gharama ya kufanya huduma hiyo ili wananchi wawatambue na
kuwa na imani nao hasa pale ambapo mzigo unapotea waweze kulipwa na
Serikali iweze kupata mapato yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment