Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, akizungumza na
waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake (hawapo pichani),
kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, mkoani Morogoro, wakati wa ufunguzi
wa semina elekezi kwa ajili ya kuwajengea ujuzi, uwezo na njia mbadala
za kuongeza idadi ya wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya
barabara.
Mratibu wa Kitengo cha
Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema
Myeya, akifafanua jambo kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa
wanawake (hawapo pichani), mkoani Morogoro, wakati wa ufunguzi wa semina
elekezi kuhusu njia mbadala za kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa
wingi katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.
Baadhi ya waratibu wa shughuli za
ushirikishwaji wa wanawake kutoka mikoa yote ya Tanzania bara
wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Meneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula,
wakati wa ufunguzi wa semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo
cha Ujenzi cha Morogoro, mkoani humo.
Mratibu wa masuala ya jinsia
kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Bi.
Diana Kahigwa akizungumza na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa
wanawake (hawapo pichani), kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, wakati wa
ufunguzi wa semina elekezi kuhusu namna ambavyo Serikali
inavyoshughulikia masuala hayo hasa katika ushiriki wa wanawake katika
kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, mkoani Morogoro.
Mratibu wa shughuli za
ushirikishwaji wa wanawake kutoka mkoa wa Shinyanga Mhandisi Jessica
Manang, akichangia mada katika semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi
wa Chuo cha Ujenzi cha Morogoro. Semina hiyo imehudhuriwa na waratibu
wa mikoa yote Tanzania bara kutoka ofisi za mameneja wa mikoa wa Wakala
wa Barabara (TANROADS).
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, akiwa katika picha
ya pamoja na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake kutoka
mikoa yote Tanzania bara katika semina elekezi iliyofanyika mkoani
Morogoro katika Chuo cha Ujenzi cha Morogoro.
……………..
Uwiano wa wanawake katika miradi
mingi ya ujenzi nchini ikiwemo matengenezo na usimamizi wa barabara
unaelezwa kufikia asilimia 6 na 7 kati ya wahandisi 100 ukilinganisha
na
wanaume katika Sekta ya hiyo.
Hayo yameelezwa na Kaimu
Meneja wa Wakala wa Barabara(TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses
Kiula, wakati akifungua semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za
ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara nchini na kufafanua
kuwa hali hiyo inatokana na ushirikishwaji mdogo wa wanawake katika kazi
hizo.
Aidha, Mhandisi Kiula,
amesisitiza umuhimu wa semina hiyo kwa waratibu hao ili kuwajengea
uwezo, ujuzi na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake
watakaoshiriki katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na pia
kuhamasisha wanawake wengine zaidi kushiriki kazi hizo.
“Serikali sasa inalenga
kuwawezesha makadarasi wanawake kufikia madaraja ya juu ya ukandarasi
ili kuweza kuinua kipato chao na kuondokana na umasikini katika familia
na jamii kwa ujumla”, amesisitiza Mhandisi Kiula.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo
elekezi yatawasaidia katika kupambanua masuala muhimu yatakayoweza
kurahisisha uratibu na usimamizi mzuri katika utendaji wa kazi za ujenzi
na matengenezo ya barabara kwa ufanisi zaidi.
“Ni maratajio yangu mkimaliza
mafunzo haya mtatekeleza kazi zenu kwa ufanisi zaidi na kuleta matokeo
chanya kwa jamii na Taifa”, amesema Mhandisi Kiula
Kwa upande wake Mratibu wa
Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi
Rehema Myeya, amesema kuwa kazi kuu za waratibu hao ni kuwahamasisha
wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za barabara katika mikoa yote
ili kutanua wigo wa maendeleo katika jamii na mafanikio katika kazi
hizo.
Mhandisi Myeya, ametaja mada
zitakazojadiliwa katika semina hiyo kuwa ni masuala ya jinsia na namna
ambavyo Serikali inayashughulikia ikiwemo sheria ya ujenzi na namna
inavyosisitiza ushiriki wa wanawake na kuipitia sheria ya manunuzi na
kuona maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.
Mada nyingine ni kuangalia
mchakato wa usajili kwa makampuni ya wanawake, kupitia mwongozo wa
kuimarisha ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara na masuala
mtambuka, namna ya kuandaa zabuni ambazo zinaakisi mahitaji ya wanawake
na ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya
barabara.
Ushirikishwaji wa wanawake
katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kitaifa ulianza mwaka
1992 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Mtwara na hii ni
kutokana na kazi hizo kufanywa na wanaume hasa kwenye nyanja za
makandarasi na wahandisi washauri.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment