Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) Bw, Richard Mayongela akifafanua jambo
kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu hawapo pichani wakati
walipokagua uwanja wa ndege wa Mwanza, kushoto ni Naibu Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John
Kwandikwa na kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS mkoa
wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya na Meneja uwanja wa ndege wa Mwanza Bi,
Esther Madale.
Muonekano wa barabara ya kutua na
kurukia ndege ambayo ujenzi wake unaendelea katika uwanja wa ndege wa
Mwanza, uwanja huo unaboreshwa ili uwe na hadhi ya kimataifa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa akifafanua
jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu
walipokagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
Muonekano wa Kivuko cha MV
Misungwi II ambacho kinajengwa na kampuni ya Songoro Marine mjini mwanza
kikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake, kivuko hicho chenye uwezo
wa kubeba abiria elfu moja na magari 36 kwa wakati mmoja kinatarajiwa
kukamilika mwezi Mei mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. John
Mongela akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu
wakipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa kivuko cha MV Misungwi II toka
kwa Bw, Mohamed Salum mwakilishi wa mkandarasi Songoro Marine
anayejenga kivuko hicho mjini Mwanza.
Mhandisi mkazi wa uwanja wa ndege
wa Mwanza Geofrey Asulumenye akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya
bunge ya Miundombinu walipokagua ujenzi wa uwanja wa ndege huo.
…………………..
Kamati ya Bunge ya Miundombinu
imeeleza kuridhishwa kwake na ujenzi wa Barabara, Kivuko na uwanja wa
ndege mkoani Mwanza na kusisitiza hali hiyo ikiendelea itawezesha
Serikali kupata huduma zinazowiana na thamani ya fedha.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.
Moshi Sulemani Kakoso amesema kamati yake imeridhika kwa hatua
zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.9, ujenzi
wa MV misungwi II na upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Mwanza.
“Hakikisheni jengo la abiria lenye
hadhi ya kimataifa linajengwa haraka katika uwanja wa ndege wa Mwanza
ili kuwiana na urefu wa uwanja huu na hivyo kuvutia ndege nyingi katika
ukanda wa Afrika Mashariki kutua Mwanza”, amesema Mhe. Kakoso.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo
Mhe. Hawa Mchafu ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA),
kuharakisha ujenzi wa uzio katika uwanja wa Mwanza ili kurahisisha
huduma za usafi, utunzaji wa mazingira na usalama wakati wote.
Nae mjumbe wa kamati hiyo Mhe.
Suzan Kiwanga amewataka wasimamizi wa miradi ya ujenzi nchini
kuhakikisha wanatoa fursa za ajira kwa wanawake pale inapoonekana wana
sifa za kufanya kazi husika ili kukuza uchumi wa jamii na kuhamasisha
wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na uhandisi.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano anaeshughulikia (sekta ya ujenzi), Mhe. Elias John Kwandikwa
amesema Serikali itaendelea kuhakikisha barabara na viwanja vya ndege
vinajengwa kwa muda mfupi ili kuokoa gharama na pale itakapohitajika
kulipa fidia kwa wananchi Serikali haitamuonea mtu.
Amesisitiza kuwa Serikali
itaendelea na sera ya kuwawezesha wakandarasi wazalendo ili kuwajengea
uwezo katika ujenzi wa miradi ya kati na mikubwa ili kukuza uchumi wa
nchi.
Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko
katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora,
Shinyanga, Simiyu, Mwanza, na Mara.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment