Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Adolf Mkenda akifafanua
jambo kwa washiriki wa kikao cha kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania
nchini Kenya mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Kuia ni Balozi wa
Tanzania nchini Kenya Dk. Pindi Chana na katikati ni Mtendaji Mkuu wa
TANTRADE Edwin Rutageruka.
Baadhi ya washiriki wa kikao cha
kujadili maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya wakimsikiliza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Prof. Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho mapema hii
leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa – MAELEZO
…………………………………………………………………………………………
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali imetoa wito kwa
wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka bidhaa zao katika soko la Kenya
ili kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao cha Maandalizi ya Wiki ya
Tanzania nchini Kenya.
Prof. Mkenda alisema kuwa ni nia
ya Serikali kuhakikisha watanzania wanapenya katika masoko ya kimataifa
ili kuongeza pato la mtu binafsi na la Taifa kwa ujumla.
“Hali ya biashara kwa sasa ni
nzuri sana, hivyo vikwazo visiwepo kabisa kati ya nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki”, alsiema Prof. Mwaikenda.
Kwa upande wake, Balozi wa
Tanzania nchini Kenya, Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kuwa watanzania
inabidi wathubutu na kuingia katika soko la Afrika Mashariki hususan
soko la Kenya.
Amesema kuwa wafanyabiashara wa
Kitanzania wasiogope kuingia katika masoko ya nje ya nchi, wajitahidi
ili waweze kuongeza vipato kutokana na ukubwa wa soko lililopo nchini na
Kenya kwa ujumla.
“Mkifanya biashara Kenya
mtaongeza mitaji, ajira na kipato kwa ujumla kwani nchi hizi mbili zina
zaidi ya watu milioni 90”, na hii inaendana na falsafa ya Mhe. Rais John
Pombe Magufuli ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatuna budi kufuata maono ya
Kiongozi wetu na kutengeneza na kuuza bidhaa za viwandani nje ya nchi”,
alisema Balozi Pindi Chana.
Akizungumza katika kikao hicho,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Juma Ali Juma amesema wazo la kufungua soko la Kenya ni zuri
na kumpongeza Balozi Pindi Chana kwa ubunifu huo.
Aliongeza kuwa anafahamu kuwa
zipo changamoto ndogo ndogo katika masoko lakini zinafanyiwa kazi ili
kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Kenya inaenda vizuri.
Bwana Juma alisisitza kuwa bidhaa
zinazozalishwa nchini inabidi ziwe na ubora na kuwa na vifungashio bora
ili kumvutia mteja kununua.
No comments :
Post a Comment