Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akizungumza na Meneja wa
Bandari za Ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese wakisafiri kwa boti ndani ya
ziwa hilo kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi
kwenye mwambao wa ziwa hilo. Aliyevaa miwani ni Meneja Uendeshaji wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akikagua upatikanaji wa huduma za
mawasiliano na uchukuzi mkoani Rukwa katika ziara yake ya kikazi mkoani
humo. Aliyeshika simu ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo Bwana Reina
Lukala
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mwalimu
Julieth Binyula akimuonesha Meneja Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard maeneo ambayo hayana
mawasiliano wakiwa kwenye bandari ya Kasanga wilayani humo wakati wa
ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta
Nditiye (hayupo pichani) ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano
na uchukuzi mkoani Rukwa
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akipata taarifa ya mkoa
wa Rukwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa mkoa huo Mhe. Joachim L. Wangapo
akiwa kwenye ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na
uchukuzi mkoani humo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akisalimiana na Meneja
wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Rukwa Bwana Peter Kuguru
alipowasili wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za
mawasiliano na uchukuzi mkoani humo
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (akiwa ndani ya gari la kwanza)
akitoka kwenye bandari ya Kasanga iliyopo ziwa Tanganyika wakati wa
ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi
mkoani Rukwa. Pembeni ni muonekano wa ziwa Tanganyika
……………………………………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kikazi ya kukagua upatikanaji wa
huduma za mawasiliano vijijini kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa
Ziwa Nyasa na Tanganyika katika maeneo ya vijiji mbalimbali viliyopo
kwenye mkoa wa Njombe, Mbeya na Rukwa.
Mhandisi Nditiye amefanya ziara
hiyo ili kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa
wananchi
waishio kwenye mwambao huo ili kujiridhisha kuhusu uwepo wa huduma hizo
ambapo Serikali kupitia Wizara hiyo inaipatia Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) ruzuku inayoziwezesha kampuni za simu za mkononi kufikisha
huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Katika ziara hiyo, Mhandisi
Nditiye amebaini uwepo wa mawasiliano hafifu kwenye baadhi ya maeneo na
mahali pengine hamna mawasiliano yoyote kwa wananchi waishio mwambao wa
ziwa Nyasa na Tanganyika. “Nimesafiri kwa boti ndani ya ziwa Nyasa
kutoka eneo la Lupingu, Ludewa mkoani Nyasa hadi matema mkoani Mbeya na
sasa kwenye bandari hii ya Kabwe mkoani Rukwa, nimeshuhudia mwenyewe
ukosefu wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa
ziwa ambapo lolote likitokea ukiwa ndani ya ziwa huwezi kabisa
kuwasiliana,” amesema Mhandisi Nditiye.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua
unuhimu wa wananchi kuwasiliana kwa kuwa mawasiliano yanachangia ukuaji
wa pato la wananchi na taifa kwa ujumla, yanawezesha na kurahisisha
shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo husika. Amesema
kuwa tayari Wizara kupitia UCSAF imefanya tathmini ya kufikisha huduma
za mawasiliano kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili
ziweze kujenga minara ya simu za mkononi.
Mhandisi Nditiye amefafanua kuwa
ukosefu wa mawasiliano haimaanishi uwepo wa minara michache ya simu za
mkononi ya kampuni fulani na ukosefu wa mnara wa kampuni mojawapo ya
mawasiliano ya simu za mkononi, bali eneo ambapo hamna mnara wa simu za
mkononi wa kampuni yoyote ile.
Ameongeza kuwa hadi hivi sasa
Serikali imefikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na
mvuto wa kibiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa kiwango cha
asilimia 94, na ni maeneo machache tu ambayo yamebaki hayajafikiwa na
huduma za mawasiliano. “Serikali imejipanga na kuhakikisha kuwa huduma
za mawasiliano zinawafikia wananchi waliosalia ifikapo mwaka 2020 ambapo
wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa Nyasa na Tanganyika wamepewa
kipaumbele hicho”, amesema Mhandisi Nditiye.
Akitoa maelezo yake kwa Mhandisi
Nditiye kuhusu mpango huo wa Serikali wa kufikisha huduma za mawasiliano
kwa wananchi waishio kwenye mwambao, Meneja wa Uendeshaji wa UCSAF
Mhandisi Albert Richard amesema kuwa, tayari Mfuko umeyabaini maeneo
hayo, kufanya tathmini ya mahitaji ya minara na fedha husika ili kuweza
kufikisha huduma za mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ya wananchi
waishio kwenye mwambao wa maziwa hayo. “Tumetembea Ludewa kwenye Tarafa
ya Mwambao yenye kata nne za Kilondo, Lumbila, Lupingu na Makonde
zilizopo mwambao wa ziwa Nyasa na kubaini uwepo wa mawasiliano hafifu na
mahali engine hakuna mawasiliano kabisa ambapo Serikali imetenga kiasi
cha dola za marekani 252,500 ambazo zitatumika kufikisha mawasiliano”.
Amesema Mhandisi Richard.
Akizungumza na Mhandisi Nditiye
kuhusu hali ya mawasiliano na miundombinu mengine kwenye mkoa huo, Mkuu
wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Andrea Tsere amesema kuwa tayari Serikali
kupitia Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) inaendelea na kazi ya
kupita kwenye eneo la mwambao wa ziwa Nyasa ili kuweza kujenga barabara
kwa kuwa wananchi waishio eneo hili hawana barabara ya uhakika. Pia,
amemshukuru Mhandisi Nditiye kwa kufanya ziara hiyo na kuzungumza na
wananchi ambapo amewahakikishia kuwa Serikali inakamilisha ujenzi wa
meli mpya kwa ajili ya eneo hilo na itajenga minara ya mawasiliano ili
kutimiza ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano inaayoongozwa na Dkt. John
Pombe Magufuli ya kuwatumikia wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhandisi
Nditiye akiwa mkoani Rukwa kwenye bandari ya Kabwe na Kasanga na bandari
ya Itungi, iliyopo Kyela mkoani Mbeya, amelielekeza Shirika la Simu
Tanzania (TTCL) kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kufunga
mitambo ya mawasiliano kwenye meli mpya ili abiria waweze kuwasiliana
wakiwa ndani ya meli kwa kuwa wengine ni wafanyabiashara wanaosafirisha
mizigo ndani na nje ya nchi kupitia maziwa hayo. Naye Katibu Tawala wa
Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya Bwana Godfrey Kawache amemueleza Mhandisi
Nditiye kuwa kuna ukosefu wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo ya kata
ya Nguna, Ngonga, Busele, Kajungumele na maeneo ya Kandete na Ibada.
Mhandisi Nditiye aliambatana na
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mwalimu Julieth Binyula na wa Nkasi Bwana
Said Mohamed Mtanda wa Mkoa wa Rukwa akiwa katika ziara yake ya kukagua
upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi katika maeneo ya mkoani
Rukwa. Bwana Mtanda amemuomba Mhandisi Nditiye kuwaelekeza wataalamu
wake kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Wilaya kutekeleza majukumu ya
Serikali kwa manufaa ya wananchi.
No comments :
Post a Comment