WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema viongozi wa Vyama vya Ushirika waliokula fedha za wakulima wa
korosho wilayani Masasi wazirudishe na wakishindwa mali zao zikiwemo
nyumba zitauzwa ili kufidia.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa ahakikishe anawasaka viongozi wa
chama Ushirika cha Msingi cha Nanyindwa wilayani Masasi ambao wamekula
fedha za wakulima na kisha kutoroka.
Amesema viongozi wa vyama vya
Ushirika katika wilaya hiyo si waaminifu, ambapo mwaka wa fedha
2016/2017 jumla ya sh. bilioni 2.3 za wakulima ziliibiwa na viongozi
hao, ambapo mwaka 2017/2018 sh. bilioni 1.7 zimeibiwa.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo
jana (Jumatatu, Februari 2018) alipozungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi pamoja na watumishi wa wilaya akiwa kwenye ziara yake ya kikazi
mkoani Mtwara.
Alisema viongozi wa Ushirika wa
Nanyindwa ambao wametoroka ni Michael Mkali, Yusuph Mataula, ambapo
alimuagiza Bw. Byakanwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola
ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu
wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuvichunguza vyama vya
Msingi katika maeneo na wakikuta kuna kiongozi amekula fedha za wakulima
wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.
Alisema wakati wa watu kuomba
kuchaguliwa kuongoza vyama vya Ushirika kwa lengo la kujitajirisha
umepita na Serikali imedhamilia inawasimamia wakulima wa mazao
mbalimbali nchini wakiwemo wa korosho ili kuhakikisha nao wananufaika.
Waziri Mkuu alisema vyama vya
Ushirika wilaya hiyo vinaongoza kwa ubadhilifu wa fedha za wakulima
ambapo wiki iliyopita Bw. Byakanwa aliwakamata viongozi 36 wa Vyama vya
Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi.
Viongozi hao ambao ni wenyeviti na
makatibu wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa
korosho ambazo ni zaidi ya sh bilioni 2.3, ambazo ni malipo ya zao hilo
kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.
Alisema mbali na
wafanyabiasharahao, pia Meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan
Msuya anaye alikamatwa kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo
ya wakulima sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.
Waziri Mkuu alimpongeza Bw. Byakanwa kwa hatua alizozichukua
dhidi ya viongozi hao na kumuagiza ahakikishe viongozi wote
waliosababisha ubadhirifu huo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya
sheria.
No comments :
Post a Comment