TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TANZANIA
YASHINDA TUZO YA TEKNOLOJIA KATIKA MKUTANO WA DUNIA WA SERIKALI (WORLD GOVERNMENT
SUMMIT 2018)
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeshinda Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World
Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka
Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).
Tuzo hiyo ilitolewa na Mtukufu
Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nchi, Ofisi ya
Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania,
UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kwa niaba ya Serikali, wakati wa kilele cha
Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini
Dubai tarehe 13 Februari 2018.
Tuzo hiyo ilitokana na
juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni
(Mikocheni Agricultural Research Institute kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo
la maradhi ya zao la muhogo “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic
Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”. Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo
ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.
Kwa kutumia teknolojia hii
mpya wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa
na wadudu, virusi, bacteria na fangasi (pathogens) kwa muda wa siku 2 tu kulinganisha
na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.
Zao la muhogo ni zao muhimu
la chakula na biashara linalotegemewa sio tu na Tanzania bali na nchi nyingine nyingi
duniani. Inakadiriwa kuwa watu wapatao
millioni 800 duniani wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo,
teknolojia hii mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na
kuendeleza zao hilo.
Nchi nyingine zilizopata
Tuzo hiyo ni India na Australia.
Wakati huo huo, Watanzania
wenye sifa wanahimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangzwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa linalohusika na masuala ya mazingira (UNEP). Nafasi inayotakiwa kujazwa
ni ya Chief Biodiversity Unit. Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika
mawasiliano http://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749
na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni tarehe 25 Februari 2018.
–Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Februari
2018. |
No comments :
Post a Comment