Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa mfumo wa ukatishaji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki
katika Meli ya MV. Clarias inayotoa huduma kati ya Mwanza na Ukerewe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akikata tiketi ya kieletroniki mara
baada ya kuzindua mfumo wa tiketi hizo katika Meli ya MV Clarias, mkoani
Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Kaimu Meneja
Mkuu wa kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamis, wakati
akikagua ukarabati wa Meli ya MV. Clarias, mkoani Mwanza.
……………………………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka kampuni ya Huduma za Meli
(MSCL) kuhakikisha inafunga kamera katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi
ili kudhibiti vitendo vya hujuma katika mifumo ya kampuni hiyo hususani
kwenye Mapato.
Ametoa rai hiyo jijini Mwanza
mara baada ya kuzindua mfumo mpya wa ukatishaji tiketi kwa njia ya
kielektroniki katika Meli ya MV Clarias na kusisitiza kuwa matumizi ya
mfumo huo mpya yaende sambamba na elimu stahiki kwa watumishi
wanaoutumia mfumo huo katika kukatisha tiketi.
“Niwapongeze sana kwa hatua hii
ya kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki katika utoaji huduma lakini
niwatake sasa kuongeza kamera kwenye maeneo yote unapofanyika ukaguzi
ili kudhibiti mianya yote inayoweza kujitokeza ya kuhujumu mapato ya
kampuni” amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali
itaendelea kuwekeza kwenye shirika hilo ili liweze kupata faida na
liweze kujitegemea na kuagiza kuwa kwa sasa kila fedha inayopatikana
itumike vizuri sababu Shirika limeanza kupata faida.
Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), kutengeneza mfumo
kama huo kwa ajili ya Shirika la Reli Nchini (TRL), ili kudhibiti
uvujaji wa mapato.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabir Kuwe, amesema mfumo huo
umetengenezwa na Wakala ili kuiwezesha taasisi hiyo kuthibiti mapato
kwani mfumo huo utarahisisha Huduma kwani abiria ataweza kukata tiketi
akiwa sehemu yoyote nchini.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL,
Bw. Erick Hamis, amesema mfumo wa kielektroniki umeanza kwa meli moja ya
MV Clarias inayofanya Safari zake kutoka Mwanza kuelekea kisiwa cha
Ukerewe ambapo katika mpango wa baadae Kampuni inategemea kutumia mfumo
huo kwenye meli zote za kampuni hiyo.
“Toka tuanze kutumia mfumo
kumekuwa na ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 20, pia na kwenye
matumizi ya mafuta hii inatupa ishara kuwa mfumo huu utatusaidia
kidhibiti mapato mengi yaliyokuwa yakipotea kwenye tiketi”amesema
Hamissi.
Ameongeza kuwa kampuni imejiwekea
mpango wa miaka miwili wa kukarabati meli Tisa za kampuni hiyo ambapo
mpaka sasa meli Tatu zimeshakarabatiwa na kuanza kazi wakati hatua ya
kuanza ukarabati kwa meli zilizobaki uko kwenye hatua mbalimbali za
manunuzi.
Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ukatishaji tiketi katika kampuni hiyo umegharimu kiasi cha shilingi takriban milioni 50.
No comments :
Post a Comment