Imeelezwa
kuwa watu wengi wanaendelea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) kutokana na kuanza mahusiano ya kimapenzi bila kutambua afya zao
hali inayosababisha waanze kuishi kama mume na mke bila kujua hali zao
za kiafya.
Hayo yamesemwa leo Februari 14,2018 na
wahudumu wa jamii wanaosaidia kazi katika vituo vya tiba na matunzo kwa
watu wanaoishi na Maambukizi ya VVU vilivyopo katika halmashauri 7 za
wilaya mkoani Mwanza yanayofanyika katika ukumbi wa hotel ya Midland
jijini Mwanza.
Wahudumu hao wapo katika mafunzo ya
msaada na huduma za kisaikolojia yanayotolewa na Shirika la Ariel Glaser
Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa ufadhili wa Watu wa
Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC).
Wahudumu walisema kitendo cha kuanza
mahusiano ya kimapenzi na kuoana bila kutambua afya ni miongoni mwa
tabia hatarishi zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuambukizana VVU.
Mmoja wa washiriki hao Chausiku Sitta
kutoka halmashauri ya wilaya ya Kwimba alieleza kuwa vijana wanapata
maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu sahihi juu ya VVU na Ukimwi
na wengi wao kutawaliwa na tamaa ya ngono isiyo salama na kudhani kuwa
kila mtu anayeonekana kuwa na umbo zuri basi hana maambukizi ya VVU.
“Vijana wanakurupuka tu,tena wakiona
mwanaume ana mvuto ama mwanamke ana makalio makubwa wao wanaita ‘wowowo’
wanachanganyikiwa kabisa,ndugu zangu huwezi kumtambua mtu mwenye
maambukizi ya VVU kwa kumwangalia kwa macho mpaka apimwe”,aliongeza Chausiku.
Naye Musa Ordas kutoka halmashauri ya
wilaya ya Buchosa aliitaka jamii kutoendekeza waganga wa jadi kwani
baadhi yao wanawadanganya watu wanaoishi na VVU kuwa wamerogwa kwa
kuwalaghai kuwa wametupiwa majini mahaba.
Kwa upande wake, Mwezeshaji katika
mafunzo hayo, Dk. Joseph Musagasa aliwataka wanaume kuacha tabia ya
kutumia majibu ya wake zao wanapopima VVU kwani majibu yanatofautiana na
hutokea wakati mwingine mmoja kati yao kuwa na maambukizi na mwingine
kutokuwa nayo.
Dk. Musagasa aliwashauri akina mama
kupima afya zao kabla ya kubeba ujauzito,na kujifungulia katika vituo
vya afya ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Siyo watoto wote wanaozaliwa na mama
mwenye maambukizi ya VVU wana VVU,hivyo mama unapotaka kubeba mimba
pima kwanza afya yako,ukibainika una maambukizi utashauriwa na wataalamu
wa afya namna ya kufanya ili usimwambukize mtoto wako”,alieleza Dk. Musagasa.
ANGALIA PICHA WAKATI WA MAFUNZO KUHUSU MSAADA NA HUDUMA ZA KISAIKOLOJIA KWA WAHUDUMU WA JAMII SIKU YA TATU
Mwezeshaji katika mafunzo ya msaada na
huduma za kisaikolojia, Dk. Joseph Musagasa akielezea umuhimu wa kupima
afya kabla ya kuanzisha mahusiano ya kimapenzi au kuingia katika ndoa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Dk. Musagasa akizungumza wakati wa
mafunzo hayo. Aliwataka watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kuzingatia
matumizi sahihi ya dawa zinazofubaza makali ya VVU pamoja na kuzingatia
lishe bora.
Chausiku Sita kutoka kituo cha afya na
matunzo cha hospitali ya Ngudu halmashauri ya wilaya ya Kwimba akielezea
namna vijana wanavyopata maambukizi ya VVU kutokana na kukosa elimu
sahihi kuhusu VVU na Ukimwi. Alisisitiza umuhimu wa kuwa muwazi
unapobainika kuwa una maambukizi ya VVU.
Musa Ordas kutoka kituo cha afya
Nyehunge kilichopo katika halmashauri ya wilaya ya Buchosa akichangia
hoja wakati wa mafunzo hayo.
Mhudumu wa afya kituo cha afya Sengabuye iliyopo katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela, Bahati Balekele Boyi.
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa Jamii
AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akielezea faida za kuzingatia lishe
bora kwamba inasaidia kuwa na afya njema.
Cecilia Yona akielezea kuhusu madhara ya kutozingatia lishe bora.
Washiriki wakijifunza kwa njia ya picha (video)
PICHA ZA MATUKIO KWENYE MAFUNZO SIKU YA PILI
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Gaston
Kakungu ambaye ni Afisa Muuguzi Mstaafu akitoa mada kuhusu umuhimu wa
kuwa muwazi unapopata maambukizi ya VVU.
Kakungu akiendelea na mada ya uwazi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya kazi za makundi.
Mshiriki wa mafunzo hayo Shija Mashimba
kutoka kituo cha tiba na matunzo cha hospitali ya Rufaa ya Bugando
akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu tabia hatarishi zinazochangia
kuwepo kwa maambukizi ya VVU,mfano kudanganywa na waganga wa kienyeji
kwa kupewa dawa za kuongeza nyota zao.
Mhudumu ngazi ya jamii, Winfrida Meshack
kutoka hospitali ya Sekouture akiwasilisha kazi ya kundi lake kuhusu
tabia hatarishi zinasobabisha maambukizi ya VVU kama vile ngoma za usiku
ambazo zinawakutanisha wanaume na wanawake.
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde1 blog
No comments :
Post a Comment