Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa
Mkoa wa Geita pamoja na Mheshimiwa Yoshida Masaharu Balozi wa Japan
Nchini Tanzania wawakifurahia jambo katika kijiji cha Kasenda mara
baada ya Makabidhiano ya Mradi wa Soko la Samaki la Kimataifa na kusaini
mkataba wa ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilometa 1 ya kutoka
Mganza kwenda Kasenda.
Mradi wa ujenzi wa Soko la
kimataifa la Samaki la Kijiji cha Kasenda Wilayani Chato uliojengwa kwa
ufadhili wa Serikali ya Japan na kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya
ya Chato.
……………………………………………………………………………….
Serikali ya watu wa Japan
imekabidhi mradi wa Soko la Samaki la kimataifa kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Chato wenye thamani ya shilingi milioni 320 na kusaini
makubaliano ya ukarabati wa barabara ya Mganza – Kasenda ili kurahisisha
usafirishaji wa mazao ya ziwani.
Akizungumza baada ya kukabidhi
mradi huo kwa Serikali Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa
Yoshida Masaharu amesema mradi huo umetolewa na Serikali ya Japan kwa
watu wa Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa urafiki wa siku nyingi katika
utekelezaji wa miradi ya kilimo na uvuvi. ”Mradi wa huu ulitolewa baada
ya kuona soko la Kasenda liko katika hali mbaya na samaki kuharibika kwa
kukosa miundombinu ya kuhifadhi ndipo Japan ikachukua hatua za haraka
kwa kutoa fedha dola za kimarekani 148,146 kwa ajili ya kujenga soko na
kukarabati soko la zamani”. Utekelezaji wa mradi ulianza mwaka 2017 na
sasa wananchi wanaendelea kunufaika.
Awali akisoma taarifa ya mradi
huo kabla ya makabidhiano mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato Joel Hari
amesema mradi unahusisha ujenzi wa ghala kubwa la kuhifadhia samaki na
ukarabati wa sokola zamani.Ameeleza kuwa soko lipo chini ya Halmashauri
ya Chato likiwa na wanachama 241 huku likikasimiwa kukusanya shilingi
milioni 140 kwa mwaka huku likitoa huduma kwa nchi za Rwanda,Burundi,
Uganda na Congo DRC.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Mkoa
wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemshukuru balozi wa Japan nchini kwa
miradi hiyo na kumwomba kuangalia na Wilaya zingine za Mkoa wa Geita ili
nazo zinufaike na miradi ya namna hiyo. Aidha, ameutaka uongozi wa
soko kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chato kuhakikisha malengo yote
yaliyokusudiwa kwa mradi huo yanatekelezeka na kuleta faida ili watu
wote wanaofanya kazi katika soko hilo waongeze kipato kwa kuwa kazi ya
Serikali ya awamu ya tano ni kujenga miundombinu bora na kuweka
mazingira wezeshi ya kusaidia kuendesha biashara.Mhandisi Robert Gabriel
ameahidi kuangalia namna ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vibanda
vya pembeni mwa soko ili kuwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Mbunge wa Chato ambaye pia ni
Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medard Kalemani amemshukuru Balozi Yoshida
kwa kutoa miradi hiyo Wilayani Chato na kuomba pia kusaidia ujenzi wa
kiwanda cha kuunganisha magari. Amewataka wananchi wa Chato na Kasenda
kutumia fursa ya uwepo wa mradi huo kujenga biashara na kutoa wito kwa
wenye mitaji midogo kuitunza ili ikuwe.Katika makabidhiano hayo Serikali
ya Tanzania na Japan zimesaini mkataba wa ukarabati wa barabara yenye
urefu wa Kilometa 1 kutoka Mganza hadi Kasenda ili kurahisisha
usafirishaji wa bidhaa za kutoka ziwani.
No comments :
Post a Comment