WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempa
mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus Yera awe
ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani
Namtumbo.
Wakazi hao 21 mwaka 2008 eneo
lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia
halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa ...
shule ya
sekondari ya mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo
jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Lwinga akiwa
katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.
Alitoa agizo hilo baada ya
kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango, ambapo
walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa
miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.
Waziri Mkuu alisema haoni
sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao sehemu ya
ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.
“Nataka wananchi hawa wawe
wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi ya mwaka huu.
Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha
maendeleo wakisumbuliwa.”
Waziri Mkuu alisema Serikali
ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtumishi
ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa
ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.
Pia Waziri Mkuu alitoa wito
kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale wanapohitaji
kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao
kuhudumiwa.
Aliwataka wananchi kuwa na
imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa
kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na
Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewataka watendaji kuhakikisha miradi wanayosimamia inakuwa na
thamani inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa na iwapo
watabainika kwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Lazima kiasi cha fedha
kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya mradi husika.
Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta mradi uliojendwa
ni wa sh. milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi tutamshughulikia
hatutamuacha salama.”
Awali, Waziri Mkuu alifungua
ghala la kuhifadhiia mpunga na mchele katika wilaya ya Namtumbo
lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na watumishi wa halmashauri
hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya
utumishi wa umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa huo unakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya mahindi
na mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula hilo linashughulikiwa
hivyo wananchi waendelee kuwa na subira.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
iJUMAA, NOVEMBA 24, 2017.
No comments :
Post a Comment