Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid
Mwanga akizungumza na vikundi mbali mbali vya wajasiriamali havipo
pichani kutoka halmashauri ya Chalinze katika halfa fupi ya
makabidhiano ya hundi yenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 120
ambayo itaweza kuwasaidia katika kufanya biashara zao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Chalinze Said Zikatimu akizungumza jambo na vikundi vya wajasiriamali
ambao walifika katika sherehe hiyo ya makabidhiano ambayo ilifanyika
katika viwanja vya sokoni Lugoba
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid
Mwanga kulia akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya kiasi cha
shilingi milioni 120 mmoja wa wanakikundi wajasiriamali katika hafla
fupi iliyofanyika katika viwanja vya soko la Lugoba
PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU
……………..
NA VICTOR MASANGU, LUGOBA BAGAMOYO
KATIKA kukabiliana na wimbi la
umasikini na ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na wanawake hatimaye
halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani imeamua
kuvipatia mikopo wa kiasi cha shilingi milioni 120 Vikundi 40 vya...
wajasiriamali kutoka kata 15 kwa lengo la kuweza kujikwamua kiuchumi na
kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi.
Akizungumza katika halfa ya
makabidhiano ya hundi kwa ajili ya fedha hizo iliyofanyika katika kata
ya Lugoba Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ambaye alikuwa mgeni
rasmi amesema lengo la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais
Dk. John Pombe Magufui ni kuhakikisha inawawezesha kiuchumi wananchi
wake pamoja na kuwapatia mikopo ya fedha kwa ajili ya kuendeshea
shughuli zao za ujasiriamali.
Aidha Mwanga aliwaagiza watendaji
na viongozi kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu vikundi vyote ambavyo
vimeshakopeshwa kufanya ukaguzi wa kina kujua fedha amabzo zimetolewa
zinatumika katika matumizi sahihi kwani amebaini kuna baadhi yao
wanakwenda kinyume na taratibu zilizowekwa hivyo kurudisha nyuma kasi
ya maendeleo.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya
Chalinze Mohamed Sume akisoma taarifa yake amebainisha kuwa fedha
hizo zote zimetokana na makusanyo yatokanayo na mapato ya ndani kwa
lengo la kuweza kuviwezesha vikundi hivyo ikiwa ni kutekeleza Agizo la
ya Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli ya kutenga asilimia
kumi kwa ajili ya kuwawezesha vijana pamoja na wanawake.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya
Chalinze Said Zikatimu amesema kuwa fedha ambazo zimetolewa katika
vikundi vya wajasiriamali hao ni katika kota ya kwanza ambapo pia
wametenga milioni 300 kwa lengo la kuweza kuvipatia vikundi vingine ili
kuweza kuongeza pato la Taifa kupitia biashara wanazozifanya.
Alisema kwamba mipango ya
halmashauri hiyo ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020 vikundi vyote
vya ujasiriamali vinawezeshwa kwa kupatiwa mikopo ya kufanyia biashara
zao mbali mbali sambamba na kuwapatiua wataalamu ambao watakuwa
wakiwafundisha namna na kuweza kujifunza masuala mbali mbali
yanayohusina na namna na kuweza kutafuta masoko katika bidhaa
wanazozizalisha.
Baadhi ya wajasiriamali ambao
wamenufaika na fedha hizo akiwemo Zawadi Rashid pamoja na Mwajuma
Shaban walieleza malengo na matarajio yao ni kuhakikisha wanakuza
mitaji yao kwa kuendeleza biashara walizonazo, ikiwemo ufugaji, kilimo,
ufyatuaji wa matofali pamoja na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ili
kuweza kujikwamua kimaisha na kukuza uchumi.
No comments :
Post a Comment