WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekabidhi zawadi ya gari aina ya carry kwa timu ya mpira wa miguu ya
Afisi Kuu Zanzibar baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya mpira
wa miguu ya Majimbo.
Mashindano hayo yaliyohusisha
majimbo 18 ya kisiwani Unguja yaliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi
Zanzibar ambayo yalizinduliwa Machi 23, 2017 na Rais wa Zanzibar Dkt.
Mohammed Shein.
Alikabidhi zawadi hiyo jana
(Jumamosi, Novemba 25, 2017) katika mechi ya fainali iliyozikutanisha
timu ya Afisi Kuu na timu ya ...
Jimbo Kwahani. Katika mechi hiyo ya fainali
Afisi Kuu iliibuka na ushindi wa magoli matatu na Jimbo Kwahani
iliambulia goli moja.
Waziri Mkuu aliipongeza CCM
Zanzibar kwa kubuni mashindano hayo ambayo yaliwakutanisha vijana.
Alisema mbali na kuimarisha afya zao pia ni chanzo cha ajira hivyo
ameishauri CCM upande wa Bara kuiga ubunifu huo.
“Ubunifu huu wa kuanzisha
mashindano ya majimbo unapaswa kuigwa na Tanzania Bara, waanzishe
mashindano haya kwa kuyakutanisha majimbo yote. Ni vema jambo hili
likawa la Kitaifa ili kunufaisha vijana wengi.”
Pia Waziri Mkuu alimpongeza
Muwakilishi wa Jimbo la Uzini, Mohammed Raza ambaye ndiye alikuwa
mdhamini mkuu wa mashindano hayo, pia aliwashauri vijana walioshiriki
mashindano hayo kuendelea kufanya mazoezi.
Katika mashindano hayo timu ya
Jimbo Magomeni ilipewa tuzo ya timu iliyoonyesha hamasa kubwa, timu ya
Jimbo Mfenesini iliibuka kidedea kwa kuongoza kwenye nidhamu na golikipa
wa timu ya Afisi Kuu, Vuai Makame Jecha alipewa tuzo ya mchezaji bora.
No comments :
Post a Comment