Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
akiwashudia wahitimu wakiwa wanavaa kofia (hawapo
pichani) baada ya kuwatunuku tuzo za fani mbalimbali kwenye mahafali
ya 31 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
amewataka Wahitimu 3108 wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini
(IRDP) waliotunukiwa tuzo
zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016/2017 kuwa
sehemu ya suluhisho katika changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi nchini
pindi watakapoanza kuwatumikia wananchi hao na siyo kuwa sehemu ya
matatizo katika jamii.
Akizungumza katika mahafali hayo ya 31 ya Chuo hicho
yaliyojumuisha Kampasi ya Dodoma na Mwanza yaliyofanyika katika ukumbi wa
Mwalimu Nyerere
Chuoni hapo Maeneo ya Miyuji mjini Dodoma Dkt. Kijaji amesema
kuwa elimu waliyoipata wakaifanyie kazi kwa uhalisia wa maisha ya Wananchi
waliopo maeneo mbalimbali ili kuliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kati hata
kabla ya 2025 kama Dira ya Taifa linavyotuelekeza.
‘Wahitimu wetu wana deni, deni hilo ni utumishi uliotukuka.
Nendeni mkawatumikie Watanzania nendeni mkairejeshe imani ya
Watanzania iliyoanza kupotea kwa Wataalam wa fani ya Mipango ya
Maendeleo Vijijini’. alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji aliongeza kwa kuwataka Wahitimu hao kwenda
kuwafundisha Watanzania kwa vitendo mipango na mbinu thabiti ili waweze
kuzalisha kwa tija kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu na ukuaji wa uchumi wa
mtu mmoja mmoja.
Aidha Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitokuwa tayari kuwavumilia Wataalamu
wazembe makazini na kuwataka wakafanye kazi kwa weledi mkubwa kwa manufaa ya
Taifa.
Dkt. Kijaji amefafanua kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha
watoto wa kitanzania wanapata elimu bora itakayowaongezea maarifa ili kuwa
chachu katika Maendeleo ya Taifa.
‘Serikali inatekeleza majukumu yake kwa vitendo, ndiyo maana
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu inapewa kipaumbele cha kwanza (first
charge). Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji ametoa wito kwa Taasisi za Elimu ya Juu zote Nchini
kutoa mafunzo yatakayowawezesha Wahitimu mbalimbali kuweza kujiajiri pindi
wamalizapo masomo yao ili kuongeza kasi ya uchumi nchini.
Katika hatua nyingine Dkt. Kijaji amekipongeza Chuo hicho kwa
utoaji wa elimu bora katika fani mbalimbali kwa kuwa idadi ya wanachuo imekuwa
ikiongezeka mwaka hadi mwaka na kwamba huo ni mfano tosha kuwa taaluma
inayopatikana katika Chuo hicho ni nzuri na kutoa rai kwa wananchi wengine
kuleta watoto wao kupata taaluma mbalimbali.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini (IRDP) Prof. Hozen Mayaya amesema kuwa wameendeleza, kuboresha na
kudumisha mahusiano bora kati ya Chuo na wadau mbalimbali.
Prof. Mayaya aliongeza kuwa ushirikiano mzuri wa wadau wao
umekuwa kichocheo kikubwa katika kutekeleza majukumu yao makuu ya kufundisha,
kufanya utafiti na kutoa huduma za ushauri na uelekezi kwa wadau mbalimbali.
‘Chuo kinajivunia kuongeza udahili wa Wanafunzi 6,129 kwa mwaka
2016/17 kutoka wanafunzi 4,916 kwa mwaka 2015/16 ikiwa ni ongezeko la asilimia
24’. aliongeza Prof. Mayaya.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack
Lokina katika hotuba yake ya kumkaribisha Mgeni Rasmi amesema kuwa Uongozi wa
Chuo umeendelea kutekeleza wajibu wake wa kuandaa wataalamu wa mipango ya
maendeleo hasa vijijini ambako watanzania wengi wanaishi.
‘Utekelezaji wa wajibu huu umeendana sambamba na kuongeza uwezo
wa Chuo katika kutoa mafunzo yanayozingatia umahiri, kufanya tafiti na kutoa
huduma za uelekezi katika Nyanja zote za mipango ya maendeleo’. aliongeza Prof.
Lokina.
Katika mahafali hayo ya 31 ya Chuo hicho jumla ya wahitimu
3,108, wanawake 1,631 wanaume 1,477 wamehitimu ngazi ya Astashahada,
Stashahada, na Shahada za Uzamili.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Wahitimu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP)
wakivaa kofia zao mara baada ya kutunukiwa tuzo mbalimbali katika
mahafali ya 31 ya Chuo hicho mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
(katikati) akiwa na viongozi wa Chuo na wageni waalikwa
katika picha ya pamoja na wahitimu wa Stashahada za
Uzamili na Shahada za Uzamili katika mahafali ya 31
ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
akihutubia wahitimu na wageni waalikwa katika mahafali ya 31 ya Chuo
Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
akimtunuku mhitimu Felista Mayunga Shahada ya Uzamili katika Uchumi
wa Maendeleo katika mahafali ya 31 ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini (IRDP) mjini Dodoma.
(PICHA NA KITENGO CHA
MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO)
No comments :
Post a Comment