Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu upasuaji wa kihistoria wa kupandikiza figo
ambao umefanyika Novemba 21, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili ikiwa ni mara ya kwanza upasuaji huo kufanyika nchini. Kushoto
ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Lawrence Museru, Dkt.
Rajesh Pande, Dkt Sunil na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya figo Muhimbili,
Dkt. Jacqueline Shoo wakiwa kwenye mkutano huo leo.
Wataalamu wa figo wa Muhimbili ambao wameshiriki katika upasuaji huo wa kihistoria wakiwa kwenye mkutano huo leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili,
Profesa Lawrence Museru akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy
Mwalimu, Dkt. Rajesh Pande na Dkt Sunil wakifuatilia mkutano huo.
Baadhi ya wataalamu wa magonjwa ya figo kutoka India wakiwa kwenye mkutano huo leo
Baadhi ya wafanyakazi wa Muhimbili na wataalamu wakifuatilia mkutano huo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya na wafanyakazi wa hospitali hiyo.
PICHA NA JOHN STEPHEN, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI
…………..
Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya New
Delhi, India imefanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa kupandikiza
figo (Renal Transplant) ikiwa ni mara ya kwanza nchini.
Upandikizaji
wa figo umefanywa na madaktari bingwa wa Mhimbili na Hospitali ya BLK
Novemba 21, mwaka huu na taarifa za wataalamu...
hao zimeeleza upasuaji huo
umekuwa wa mafanikio makubwa na kwamba utakuwa endelevu.
Akizungumza
katika mkutano wa waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kufanyika kwa
upasuaji huo ni moja ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuboresha na
kuanzisha huduma bora za kibingwa nchini.
“Serikali
inaendelea na juhudi za kuboresha huduma za afya nchini chini ya Rais
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli zikiwamo za kibingwa nchini na kupunguza
rufaa za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo nje ya nchi,” amesema Ummy
Mwalimu.
Amesema
upasuaji figo katika Hospitali ya Muhimbili utasaidia kupunguza gharama
kubwa ambazo serikali imekuwa ikitumia kupeleka wagonjwa nje ya nchi.
Waziri
huyo amesema hivi sasa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo na
kwamba takwimu zinaonesha Muhimbili kuna wagonjwa 200 wanaofanyiwa
huduma ya utakasishaji damu.
Amesema
kutokana na ongezeko hilo, Serikali imeanzisha vituo vya utakasishaji
damu katika hospitali za Mbeya Rufaa, Benjamin Mkapa, KCMC, Bugando na
hospitali binafsi zikiwamo Kairuki, TMJ, Regency na Hindu Mandal.
“Kwa
namna ya pekee nawashukuru wataalamu 11 ambao tupo nao hapa wakiongozwa
na Profesa. H.S. Batyal, Dkt. Sunil Prakash, Dkt. Rajesh Kumar Pande na
Dkt. Anil Handoo ambao kwa kushirikiana na wataalamu wetu wamefanikisha
upasuaji huu. Pia, napenda kuwashukuru wakurugenzi, wataalamu pamoja
na Wafanyakazi wote wa Muhimbili wakiongozwa na Prof. Lawrence Museru,”
amesema.
Naye
Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema kuwa mpango wa
kupandikiza figo umewezeshwa na hospitali hiyo ikiwa ni utekelezaji wa
mikakati ya kuboresha huduma za afya nchini.
Profesa
Museru amesema awali ilipeleka India wataalamu kwa ajili ya kupata
mafunzo ya kutekeleza mradi huo na kwamba umekuwa wa mafanikio makubwa
nchini Tanzania.
Mkurugenzi
huyo amesema mpango huo utasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa
waliokuwa wanapelekewa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya figo.
Profesa
Museru amesema upandikizaji wa figo ambao unajumuisha kumuandaa
mgonjwa, vipimo mbalimbali vinavyohitajika kwa mpokeaji na mtoaji figo
unagharimu wastani wa Sh. 21 milioni za kitanzania katika hospitali hiyo
ya Muhimbili.
“Hii
ni nafuu sana ukilinganisha na gharama ya Sh.80 hadi 100 milioni
iliyokuwa ikitumiwa na Serikali kupeleka mgonjwa mmoja nje kwa huduma
hii ikiwamo matibabu, usafiri na malazi. Hivyo basi, licha ya huduma hii
kusaidia kuleta huduma za kisasa nchini pia, itakuwa ni nafuu sana na
kuwezesha wagonjwa wengi zaidi kupatiwa huduma hiyo,”amesema Profesa
Museru.
Mkurugenzi
huyo amesema kuwa mafanikio ya upasuaji huo utasaidia kuweka msingi wa
kuanzisha programu nyingine za upandikizaji viungo (organ transplant) hapa nchini kama vile upandikizaji wa ini (liver transplant).
“Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wataalamu kutoka Hospitali ya BLK New
Delhi, India ambao wameshirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
zaidi ya mwaka mmoja katika mipango na maandalizi ya utoaji wa huduma ya
upandikizaji figo. Kwa namna ya pekee nawashukuru hawa wataalamu 11
ambao tupo nao hapa wakiongozwa na Profesa H.S. Batyal, Dkt. Sunil
Prakash, Dkt. Rajesh Kumar Pande na Dkt. Anil Handoo ambao kwa
kushirikiana na wataalamu wetu wamefanikisha upasuaji huu,” amesema
Profesa Museru.
No comments :
Post a Comment