Mkurugenzi wa Miradi Endelevu wa
Mfuko wa Abbott, Dkt. Festo Kayandabila akieleza jinsi mfuko wa Abbott
ulivyoshiriki kuwapatia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kadi
za bima ya afya. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili,
Profesa Lawrence Museru, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mkuu wa Kitengo cha Wateja
Binafsi, Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati wa benki ya ABC, Joyce Malai
na Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Kurasini, Rabikira Mushi.
…………..
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeupongeza mfuko
wa Abbott kutokana na juhudi kubwa za kusaidia kuboresha huduma ya afya
katika sekta ya afya nchini.
Kauli
hiyo imetolewa Leo na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu kabla ya
kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto 139 wanaoishi katika mazingira
magumu.
Mfuko
huo kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na benki ya
ABC, leo wamekabidhi kadi kwa watoto hao kupitia Waziri Ummy Mwalimu.
“Napenda
kuupongeza Mfuko wa Abbott kwa kuwezesha watoto hawa 139 kupata kadi za
bima ya afya, hongereni sana. Nimeambiwa Kadi hizi mmezilipia na
zitaisha baada ya mwaka mmoja, hivyo naomba muendelee kuzilipa endapo
haitawezekana Serikali italipa, lakini naamini kwamba hamtashindwa
kuendelea kuiunga mkono Serikali,” alisema Waziri Ummy Mwalimu.
Baada
ya Waziri huyo kutoa kauli hiyo, Mkurugenzi wa Miradi endelevu wa Mfuko
wa Abbott, Dkt. Festo Kayandabila alisema kuwa wako tayari kuwasaidia
watoto hao.
Mfuko
wa Abbott umekuwa ukiisaidia Hospitali ya Taifa Muhimbili katika juhudi
zake za kuboresha huduma za afya. Mfuko huo umesaidia kukarabati Idara
ya Magonjwa ya Dharura na Ajali pamoja na kukarabati Jengo la maabara
kuu.
No comments :
Post a Comment