1.
Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea
na kujadili Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na
Bajeti kwa Mwaka 2018/19.
2.
Mheshimiwa Spika, awali
ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na
afya. Aidha, tunamshukuru sana kwa kuendelea kulijalia Taifa letu amani na
utulivu na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa tisa wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya nchi
yetu.
3.
Mheshimiwa Spika, kipekee napenda
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na
Mipango kufuatia mabadiliko aliyoyafanya hivi karibuni katika Baraza lake la
Mawaziri na safu ya uongozi wa Mikoa. Aidha, ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri,
Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa waliobakia katika nafsi zao na wale
waliobadilishwa vituo vya kazi. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati wote
walioteuliwa kuwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa wapya.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba
pia nitumie fursa hii adhimu kutambua na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri na
makini katika kusimamia rasilimali za Taifa, kupambana na rushwa, kuimarisha nidhamu
na uwajibikaji katika utumishi wa umma na zaidi ya yote, kwa moyo wake adili
katika kupatia majibu kero za wanyonge. Hakika uongozi wake umezidi kuijengea
heshima kubwa nchi yetu.
5.
Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie fursa hii kumpongeza Mhe.
Janeth Masaburi (Mb) aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge katika Bunge
lako Tukufu hivi karibuni kutoka Chama Tawala cha CCM. Aidha, nawapongeza kwa
pamoja Waheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Kiza Hussein Mayeye, Nuru Awadh
Bafadhili, Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Sonia Jumaa Magogo, Rehema
Juma Migilla na Zainab Mndolwa Amir walioteuliwa na Chama cha Wananchi - CUF
kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninapenda kuwakaribisha
na kuwashauri watumie jukwaa hili kikamilifu katika kuishauri Serikali na
kuwatumikia wananchi. Napenda pia kumpongeza Bw. Stephen Kagaigai kwa kuteuliwa
na Mheshimiwa Rais kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
6.
Mheshimiwa Spika, ninawiwa
pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa
Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb) na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na
Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano
walionipa katika maandalizi ya hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango
na Mwongozo. Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali,
Sekta Binafsi na wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika
kukamilisha Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.
7.
Mheshimiwa Spika, hoja ninayoiwasilisha
hapa imetayarishwa kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa jamii. Kwa
ujumla tumepata maoni na ushauri kutoka katika makundi mbalimbali ya jamii na
Taasisi za Serikali. Siwezi kuwataja mmoja mmoja wale wote waliochangia hoja
hii hadi kufikia hapa. Hata hivyo, kwa namna ya kipekee, napenda kuishukuru na
kutambua mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti
wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini katika
kuboresha rasimu za Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka
2018/19 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2018/19. Maoni
na ushauri mahsusi wa Kamati ulijikita katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja
na yafuatayo:
(i)
Kujumuisha
matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na kama malighafi
katika viwanda ikiwemo viwanda vya mbolea;
(ii)
Kuzingatia
maeneo yanayogusa wananchi walio wengi kwa ajili ya kukuza kipato na kupunguza
umaskini hususan kilimo, uvuvi, upatikanaji wa pembejeo na mitaji;
(iii) Kuweka msukumo mkubwa katika kuboresha mazingira kwa
ajili ya ushiriki wa Sekta Binafsi katika kugharamia na kutekeleza miradi ya
maendeleo inayolenga kutimiza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda na
maendeleo ya watu;
(iv) Kuendelea kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa
mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya;
(v) Kuendelea kulipa madeni yaliyohakikiwa na kuzuia
uzalishaji wa madeni mapya; na
(vi) Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) kwa kipindi cha miaka miwili ya awali.
No comments :
Post a Comment