|
WAZIRI
wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango amesema serikali itaziwajibisha taasisi
zote zilizobainika kufanya vibaya katika manunuzi yake ya mwaka 2016/17 kwa mujibu
wa sheria ikiwa ni pamoja na wote waliohusika kufikishwa mbele ya vyombo vya
dola ikiwemo Takukuru kwa uchunguzi zaidi.
Dkt.
Mpango amesema hayo leo mjini Dodoma mara baada ya kupokea Ripoti ya Tathmini
ya Utendaji ya PPRA kwa mwaka wa fedha 2016/17 ambayo pamoja na mambo mengine
muhimu, inajumuisha matokeo ya ukaguzi wa manunuzi yaliyofanywa na taasisi za
umma katika mwaka husika. Ukaguzi huo ulihusisha Taasisi za Umma 112.
Ripoti
hiyo inaonesha baadhi ya taasisi kufanya malipo yenye utata/hewa ambazo ni
pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) na Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ambapo kiasi cha shilingi milioni
483.44 zililipwa kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazikuwa zimefanyika.
Aidha, Ripoti hiyo imeonesha kuwepo kwa
taasisi sita zilizofanyiwa uchunguzi na kubainika kuisababishia Serikali hasara
kubwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo;
ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi uliosababisha ongezeko la riba, pamoja
na faini zilizotokana na ukiukwaji wa taratibu za kijamii na mazingira kabla ya
kuanza kwa utekelezaji wa kazi za ujenzi. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Taasisi ya Mifupa (MOI), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
(TCRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Wizara ya Fedha na Mipango, pamoja
na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
“Naahidi
kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Ripoti hii na ni lazima tuhakikishe
kuwa fedha za umma zinalindwa kwa nguvu zote. Kila mtu aliyehusika
kuisababishia Serikali hasara ni lazima atawajibika na sheria lazima isimamiwe
kwa ukamilifu,” alisema Waziri.
Pia,
Waziri Mpango aliongeza kuwa kwa zile taasisi zilizobainika kuwa na viashiria
vya rushwa wahusika wote watajieleza na pia watawasilishwa Takukuru kwa
uchunguzi zaidi na mamlaka za uteuzi na baada ya hapo hatua stahiki
zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi ya PPRA, Dkt. Balozi Matern
Lumbanga alisema kuwa ripoti imejumuisha matokeo ya ukaguzi uliofanywa na PPRA
kwa taasisi nunuzi ili kupima kiwango cha uzingatiaji sheria na pia upatikanaji
wa thamani ya fedha ambapo jumla ya taasisi nunuzi 112 zilifanyiwa ukaguzi huu.
Aidha,
Balozi Lumbanga aliongeza kuwa matokeo ya ukaguzi wa uzingatiaji sheria
yanaonesha kuwa wastani wa uzingatiaji kwa taasisi zilizokaguliwa ni asilimia
74 ambayo ni ongezeko la asilimia moja ikilinganishwa na wastani wa mwaka
uliopita ambao ulikuwa asilimia 73.
Kwa
upande mwingine, taasisi 81 kati ya 112 zilifanyiwa ukaguzi wa kupima thamani
halisi ya fedha. Jumla ya mikataba ya miradi 345 ilikaguliwa ambapo miradi 87
ilipata alama za kiwango cha kati/kawaida, na saba ilipata alama za kiwango
kisichoridhisha.
“Miradi
iliyopata kiwango kisichoridhisha inajumuisha miwili ya ujenzi wa majengo yenye
thamani ya shilingi 201.542 milioni, mradi mmoja wa ujenzi wa barabara wenye
thamani ya shilingi 146.92 milioni, miradi miwili ya ujenzi yenye thamani ya
shilingi 405.63 milioni. Mingine ni mmoja wa huduma za ushauri wa kitaalam
wenye thamani ya shilingi 25.46 milioni, na mradi mmoja wa usambazaji wa maji
wenye thamani ya shilingi 1.59 bilioni” alisema Balozi Lumbanga.
Kuhusu
viashiria vya rushwa, PPRA pia ulipima uwezekano wa uwepo wa rushwa katika
taasisi au miradi husika. Tathmini ya jumla ya viashiria vya rushwa ilionesha
kwamba miradi 33 katika taasisi 17
ilibainika kuwa na kiwango kikubwa cha viashiria vya rushwa ikimaanisha kuwepo
kwa uwezekano mkubwa wa uwepo wa vitendo vya rushwa katika taasisi na miradi
hiyo.
Taasisi
hizo ni Mamlaka za Maji Safi na Maji Taka za Moshi (Muwasa), Mwanza (Mwauwasa)
na Arusha (Auwasa); pamoja na Halmashauri za Wilaya za Msalala, Kibondo na
Moshi. Taasisi nyingine ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela,
Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Chuo cha Ufundi Arusha, Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Ofisi
ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Mji wa Masasi, pamoja na Kituo cha
Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Ripoti
hii ni ya 11 tangu PPRA ilipoanzishwa. Ripoti hii inatoa tathmini ya utendaji
ambapo imeelezea kwa kina kazi mbalimbali zilizotekelezwa na PPRA katika
kusimamia shughuli za ununuzi wa umma katika mwaka wa fedha 2016/17 ambapo
pamoja na mambo mengine, ni pamoja na Ujengaji uwezo kwa taasisi nunuzi,
Usimamizi wa mifumo ya habari za ununuzi, Utoaji huduma za ushauri katika
ununuzi na pia kusimamia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410.
|
No comments :
Post a Comment