NA
BENEDICT LIWENGA-WHUSM, KAMPALA-UGANDA.
MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Bibi Leah
Kihimbi amesema kwamba, Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki maarufu
kama JAMAFEST limesheheni vionjo mbalimbali vinavyoelezea uhalisia wa utamaduni
wa nchi Wanachama za Afrika Mashariki.
Kauli hiyo ameitoa leo mjini Kampala nchini Uganda
katika muendelezo wa Tamasha hilo ambapo amefafanua kuwa, kupitia tamasha hilo
washiriki kutoka Tanzania wamejifunza mambo mengi yakiwemo mavazi, vyakula na
baadhi ya bidhaa ambazo baadhi ya nchi hazipatikani jambo ambalo amesisitiza
kuwa, Viongozi waanzilishi wa tamasha hilo hawanabudi kuliendeleza kwakuwa
linatoa fursa ya kuleta maendeleo na kukuza mahusiano.
“Idara ya Sanaa na Utamaduni sasa itakuwa na mkakati
madhubuti ambao utajikita katika kupata vikundi bora mbalimbali kupitia mambo
tuliyojifunza toka kwa wenzetu, lakini pia tunawashukuu sana wajasiriamali kwa
kuleta bidhaa mbalimbali mbazo ni tofauti kwakuwa baadhi vimekuwa havipatikani
sehemu nyingine, na pia kwa upande wa vikundi vya Tanzania nimeshuhudia moja ya
kikundi cha Rwanda kikijifunza moja ya ngoma toka kwa kikundi chetu cha
Tanzania hakika tamasha hili ni muhimu sana kwetu sisi na kwa wenzetu”, alisema
Kihimbi.
Ameongeza kuwa, katika burudani zilizotolewa na
baadhi ya nchi wanachama zimekuwa na vionjo adimu kama vile vichekesho, ngoma
za kitamaduni pamoja na mavazi ya asili jambo ambalo limewavutia washiriki
wengi huku akitoa msisitizo wa kutunza tamaduni za nchi wanachama kwa ajili ya
maendeleo ya nchi hizo.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Maigizo toka Taasisi ya
Sanaa na Utamaduni (TaSUBA), Bibi, Christa Komba amesema kuwa, kwa upande wao
wamekuja na igizo la ‘Mti’ ambalo maudhui yake yamejikita katika kusisitiza
kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaungana kwa pamoja katika
kufanya kazi pamoja kwa maendeleo ya pamoja hususani katika nyanja za sanaa na
utamaduni.
“Maudhui ya igizo letu la mti ni kuonyesha kwamba
hakuna mtu mwenye thamani kuliko mwingine kwakuwa yatupasa kufanya kazi kwa
pamoja kwa maendeleo yetu kwa pamoja”. Alisem Bibi Christa.
Ameongeza kwamba, sanaa endapo ikitumika vema katika
jamii yoyote ina nguvu katika mawasiliano na inasaidia kuboresha maendeleo ya
jamii yoyote.
Tamasha la JAMAFEST lilianzishwa mwaka 2013 nchini
Rwanda ambapo hufanyika kila baada ya miaka miwili baina ya nchi wanachama za
Afrika Mashariki ambapo kaulimbiu ya tamasha hilo kwa mwaka huu inasema kwamba
‘Utamaduni na Ubunifu, Kiini cha Ajira na Umoja’.
Mshiriki
kutoka Jamhuri ya watu wa Burundi (kushoto) akiangalia moja ya nguo aliyoipenda
katika moja ya mabanda ya Tanzania katika muendelezo wa Tamasha la Utamaduni na
Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linaloendeleo mjini Kampala, Uganda 13
Septemba, 2017.
Mkurugenzi
wa Sera na Mipango wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Petro
Lyatuu akiangalia baadhi ya bidhaa toka kwa Wajasiriamali katika banda la
Watanzania mjini Kampala wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika
Mashariki (JAMAFEST) linaloendelea mjini Kampala nchini Uganda 13 Septemba,
2017.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Bibi Leah Kihimbi (kulia) akiangalia baadhi ya bidhaa toka kwa Wajasiriamali katika banda la Watanzania mjini Kampala wakati wa Tamasha la Utamaduni na Sanaa Afrika Mashariki (JAMAFEST) linaloendelea mjini Kampala nchini Uganda 13 Septemba, 2017.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
No comments :
Post a Comment