MKUU wa Wilaya ya Mkalama mkoani
Singida, Eng. Jackson Jonasi Masaka, amewaagiza madereva wa boda boda
kuanzisha na kusajili vikundi vya ujasiriamali, ili ...
kujijengea mazingira
mazuri kupata mikopo toka tawi la NMB benki, lililozinduliwa wilayani
humo. Eng. Masaka ametoa agizo hilo juzi wakati akizungumza kwenye
uzinduzi rasmi wa tawi la NMB tawi la Mkalama, lililopo katika makao
makuu ya wilaya hiyo, Nduguti.
Alisema kufunguliwa kwa tawi hilo
kumesogeza karibu zaidi huduma mbalimbali ikiwemo ya mikopo zinazotolewa
na NMB benki, kwa wakazi wa wilaya hiyo. Akifafanua, alisema huko nyuma
wakazi wa wilaya hiyo pamoja na watumishi wa umma, iliwabidi kufuata
huduma za kibenki Singida mjini, umbali wa kilometa 140 kwenda na
kurundi.
“Kwa hiyo ninyi madereva wa
bodaboda, NMB imesongeza huduma…huu ni wakati muafaka kuboresha shughuli
zenu. Msilale changamkeni, jiungeni kwenye vikundi vilivyosajiliwa
muweze kupata mikopo itakayokuza mitaji yenu. Mjue tu kwamba dereva
mmoja mmoja ni ngumu mno kupata mkopo kwenye taasisi za kifedha”,
alisema mkuu huyo wa wilaya. Eng. Makata pia ametumia fursa hiyo
kuwahamasisha baba/mama lishe, wauza chips na wajasiriamali mbalimbali
wakiwemo wadogo, kuchangamkia mikopo kupitia akaunti ya ‘FANIKIWA’.
“Niipongeze NMB benki kwa kubuni
bidhaa hii ya akaunti ya FANIKIWA. Kupitia akaunti hii ya FANIKIWA,
wajasiriamali niliowataja hapo juu, wataweza kupata mikopo kati ya
shilingi laki tano na milioni 30. Nasisitiza tumieni fursa hizi
zilizosongewa karibu zaidi na NMB, ili mkuze mitaji yenu iweze kukidhi
mahitaji ya wakati wa sasa,” alisema.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo
wa wilaya ameishukru na kuipongeza NMB benki kwa msaada wake wa vitanda
15, magodoro 15, vitanda viwili vya kujifungulia akina mama wajawazito
na mashine mbili za kupimia mapigo ya moyo.
“Msaada huu wenye thamani ya
shilingi milioni 10 ambao umetolewa kwa kituo cha afya, vitunzwe na
kulindwa vizuri ili viweze kutumika kwa kipindi kirefu,” alisema Eng.
Makata. Awali meneja wa uhusiano wa biashara kati ya serikali na benki
NMB kanda ya kati, Yasin Mfinanga, alisema msaada huo ni mwendelezo wa
NMB katika kumuunga mkono Rais Dk. Magufuki kuboresha sekta ya afya.
“Kila mwaka baada ya kutoa gharama
zote za uendeshaji, benki yetu huwa inatenga asilimia moja ya faida,
kwa ajili ya kutoa misaada inayolenga sekta ya afya na elimu. Agizo la
rais Magufuli la kuchangia madawati katika shule za msingi na sekondari,
NMB ilishiriki kikamilifu,” alisema Mfinanga kwa kujiamini.
Mfinanga alitumia fursa hiyo
kuwataka wakazi wa kanda ya kati, kuacha kabisa utamaduni wa kutunza
fedha kwenye simu zao za viganjani na badala yake wazitunze kwenye
mabenki ikiwemo ya NMB. Akisisitiza, alisema fedha zinazotunzwa kwenye
simu za viganjani usalama wake ni mdogo mno, ikilinanishwa na zile
zinazotunzwa kwenye mabenki ya kuaminika.
“Fedha hizi zilizopo kwenye simu
za viganjani na wakazi wa kanda ya kati wakijitokeza kwa wingi kuweka
fedha benki, hatua hiyo itachangia NMB benki kuwa na uwezo mkubwa katika
kutoa mikopo. Aidha, hatua hii itachangia benki kupunguza riba
zinazokatwa kwenye gharama za uendeshaji,” amesisitiza zaidi.
Wakati huo huo.mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mkalama, James Mkwega, alisema kufunguliwa kwa
tawi la NMB tawi la Mkalama, pamoja na mambo mengine, kutachochea ukuaji
wa uchumi. “Binafsi nimefarijika mno…na naipongeza NMB benki kufungua
tawi hapa kwetu Nduguti makao makuu ya wilaya ya Mkalama. Huko nyuma
tulilazimika kufuata huduma za kibenki Singida mjini kilometa 140 kwenda
na kurudi. Madhara yake yalikuwa makubwa mno,” alisema na kuongeza;
“Watumishi wa umma wakiwemo walimu
nao wametaabika sana katika kufuata mishahara yao New Kiomboi wilaya ya
Iramba umbali wa likometa 90. Hapo ilikuwa kabla wilaya Iramba
yaijagawanywa na kuzaa wilaya ya Mkalama. Nakumbuka baadhi ya walimu
walikuwa wanatumia usafiri wa baiskeli, wakifika msitu wa Gumanga,
walikuwa wakiporwa mishahara yao na majambazi,”
Mwenyekiti huyo ambaye ni diwani
(CCM) kata ya Gumanga, alisema kuwa kwa sasa hayo yote yatabaki kuwa
histori, baada ya NMB kufungua tawi hilo.
No comments :
Post a Comment