Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefuta umiliki wa mashamba matano
yenye jumla ya hekari 14,000 yaliyoshindwa kuendelezwa na wamiliki wake
katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Hatua hiyo imechukuliwa leo na
Rais Magufuli wakati ...
akiwahutubia wananchi wa Wilaya hiyo alipokuwa
anapita kuelekea Tanga kwa ajili ya shughuli ya uwekaji wa jiwe la
msingi katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka
Hoima nchini Uganda hadi Tanga,Tanzania.
Rais amefuta umiliki huo baada ya
baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo waliopewa mashamba hayo kwa ajili ya
kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kilimo ambacho kingeiingizia
Serikali mapato, kuyaacha maeneo hayo bila kufanya uwekezaji tarajiwa.
“Tayari nimeshafuta umiliki wa
mashamba matano yaliyokuwa yamechukuliwa bila kuendelezwa, nimeyarudisha
kwa uongozi wa Mkoa ili wayapange maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za
Serikali pamoja na kuyagawa kwa wananchi. Nasisitiza wananchi wagaiwe
mashamba hayo bure,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameongeza kuwa ardhi
ya mkoa wa Tanga haikupangwa kwa ajili ya wawekezaji bali ni ardhi kwa
ajili ya wananchi wote hivyo wana haki ya kupewa bure ardhi hiyo
iliyoshindwa kuendelezwa.
Katika safari hiyo ya kuelekea
Tanga mabapo alisimama maeneo mbalimbali kuwahutubia wananchi, Rais
Magufuli alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel
kwa kutumia vizuri fedha za Serikali kuhamasisha vikundi vya wananchi
kujenga madarasa kwa gharama ndogo na kuwataka viongozi wengine kuiga
mfano wake.
Alipopewa nafasi ya kuwasalimia
wananchi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu alisema kuwa utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais
Magufuli unaonesha wazi dhamira yake ya kutaka kuifanya Tanzania kuwa
mpya hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha hamkatishi tamaa Rais
Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa
juhudi zake za kuibadilisha Tanzania, katika bajeti ya sekta ya afya ya
mwaka huu, tumepewa shilingi milioni 650 kwa ajili ya kuimarisha kituo
cha afya cha Mkuzi, kikubwa ninaomba mtusaidie kuwaibua wanaouza dawa za
Serikali ili tukomeshe tabia hii,” alisisitiza Waziri Ummy.
Baadhi ya maeneo ambayo Rais
alisimama kuongea na wananchi wakati akielekea Tanga ni pamoja na Mkata,
Michungwani, Hale, Muheza na Mkanyageni.
Rais Magufuli pamoja na Rais
Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda wanatarajiwa kuweka Jiwe la Msingi
katika mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini
Uganda mpaka Tanga, Tanzania. Jiwe hilo la msingi litawekwa eneo la
Chongoleani lililopo Barabara ya Horohoro kuelekea Mombasa nje kidogo ya
jiji la Tanga.
No comments :
Post a Comment