HAFLA YA UZINDUZI WA TAWI LA NBM HAYDOM MKOA WA MANYARA
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya
ya Hanang akizindua jengo la tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa
Haydom. Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya
ya Hanang (wa tatu kulia) kikata utepe kuashiria uzindua wa jengo la
tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa Haydom. Wa pili kulia ni Meneja
wa NMB Kanda ya Kati, Straton Chilongola.[/caption]
KILIO cha wakazi wa jimbo la Haydom wilaya ya Mbulu mkoani
Manyara cha kukosa huduma za kibenki toka Tanzania ipate uhuru,kimepata
ufumbuzi wa kudumu baada ya NMB benki, kufungua tawi katika mji mdogo wa
Haydom. Kwa mujibu wa mbunge wa jimbo la Haydom, Flatei Massay, katika
kipindi chote hicho, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakilazimika
kufuata huduma za kibenki Mbulu mjini, umbali wa zaidi ya kilometa 90.
Mbunge Massy alisema kitendo cha kufuata huduma za kibenki umbali mrefu
kiasi hicho, kumekuwa na madhara mengi na makubwa, ikiwemo gharama kubwa
ya usafiri na pia usalama wa fedha.
“Umbali huo umesababisha wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa
ujumla, kutunza fedha zao majumbani. Miaka ya nyuma majambazi yalitumia
bomu kubomoa kasiri (sefu) la kutunzia fedha mali ya hospitali ya rufaa
ya misioni Haydom na yalifanikiwa kuiba fedha, Pia fedha nyingi
ziliungua kwa moto wa bomu”, alisema na kuongeza;
“Zipo hisia kwamba majambazi hayo yalihisi hospitali hiyo haipeleki
fedha benki kwa wakati kutokana na umbali mrefu benki ilipo, kwa hali
hiyo yalitarajia kupata fedha za kutosha”.
Mbunge huyo alisema kufunguliwa kwa benki hiyo yenye mashine mbili za
kutolea fedha, wananchi na wafanyabiashara, wanapaswa kuitumia
kikamilifu, ili kupanua kilimo na biashara zao.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufunguzi huo, kaimu mkuu wa mkoa wa
Manyara, Sara Msafiri Ally, ameihimiza benki ya NMB kuongeza juhudi
zaidi katika kuendelea kutoa mikopo na huduma zingine kwa wakazi wa
vitongoji vyote mkoani Manyara. Alisema serikali ya awamu ya tano
imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini, hivyo mikopo inayotolewa
na mabenki ikiwemo NMB, itasaidia kuendeleza kukuza uchumi na kuongeza
ajira.
Ameongeza kwa kuwahimiza wananchi wa Haydom, kuchangamkia uwepo wa benki
ya NMB, ili kutumia huduma zao za kibenki kupata maendeleo yao binafsi,
wilaya ya Mbulu na mkoa wa Manyara kwa ujumla.
“Serikali inawapongeza NMB kwa kutambua umuhimu wa kusaidia jamii. Ni
ulweli usiofichika kuwa faida mnayopata katika huduma zenu za kibenki,
inatokana na wananchi. Hivyo kusaidia jamii ni njia nzuri ya kurudisha
shukrani kwa waliosaidia mkapata faida”, alifafanua Sara.
Awali meneja wa NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, alisema NMB tawi
la Haydom, litahudumia vijiji na viitongoji vya Maghani, Labai,
Maritadu, Endamilayi, Getanyamba na Dongobeshi. Aidha, alisema benki
hiyo imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye kuzingatia mahitaji
halisi ya soko kwa wakati husika.
“Moja ya bidhaa hizo, ni kampeni ya ‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni
mahususi kabisa kwa wajasiriamali wadogo wadogo. Wajasiriamali hao ni
pamoja na baba/mama lishe, wauza chipis, wenye maduka ya biashara
yakiwemo ya nguo”, alifafanua Chilongola.
Akifafanua zaidi,alisema akaunti hiyo inampa fursa mteja kupata mkopo wa
shilingi laki tano hadi shilingi 30 milioni. Pia meneja huyo, alisema
wanayo akaunti nyingine ya ‘Wajibu’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya
watoto wenye umri wa miaka 0-18.
“Kwa upande wa teknolojia, tuna akaunti ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii
mteja anaweza kufungua akaunti kwa muda mfupi na papo hapo kupata kadi
yake ya ATM, na kuanza kufanya miamala wo wote”, alisema Chilongola.
Benki ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na mashine za kutolea fedha zaidi
ya 700 nchi nzima.Ina wateja zaidi ya milioni mbili jambo linaloifanya
kuwa benki pekee nchini yenye hazina ya wateja wengi kuliko benki
zingine zilizopo nchini.
No comments :
Post a Comment