| Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimpongeza kwa furaha mmoja wa mwanajeshi aliyehusika kusafirisha Madawati 2579 yaliyotolewa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Madawati hayo yamefikishwa Singida kwa ajili ya urahisi wa kuyasambaza katika mikoa hiyo. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akishirikiana na wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) na Askari wa Magereza kushusha madawati yalitolewa na
Bunge. Madawati hayo 2579 yanapelekwa katika mikoa ya Manyara, Arusha na
Kilimanjaro.
Askari wa Magereza wakipanda moja
ya magari ya JWTZ na kusaidia kushusha sehemu ya madawati 2579
yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa niaba ya mikoa ya Arusha,
Manyara na Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi akipokea kwa furaha moja ya magari ya Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) yaliyokuwa yamebeba Madawati hayo 2579 yanapelekwa
katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Madawati hayo yametolewa
na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
………………………………………………………………..
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.
Rehema Nchimbi leo ampokea madawati 2579 kutoka kwa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa niaba ya mikoa ya Manyara, Arusha na
Kilimanjaro.
Akipokea madawati hayo
yaliyosafirishwa katika magari 19 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) Dkt Nchimbi amelipongeza jeshi hilo kwa uzalendo huo wa
kuhakikisha mali za umma zinafika Singida kwa ajili ya kuanza kusambazwa
katika halmashauri husika zikiwa salama na katika hali nzuri.
Dkt Nchimbi amelipongeza Bunge
kwa uzalendo wa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli katika kuhakikisha sekta ya elimu inaboreka
nchini ili kutimiza azma ya kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Amesema madawati hayo yataongeza
motisha kwa wanafunzi kujisomea kwakuwa mazingira yatawawezesha kuandika
na kusoma kwa ufanisi zaidi.
Aidha Dkt Nchimbi amezitaka
halmashauri zitakazopokea madawati hayo kuhakikisha wanayatunza ili
yadumu na kuwanufaisha wanafunzi kwa muda unaostahili.
“Madawati na yenyewe yanahitaji
ukarabati, sio kwakuwa mmepewa basi muyaache tu, hapana, ukiona ubao
unalegea kidogo basi hakikisha unarekebisha na sio kuanza kusubiri
waliotupatia ndo waturekebishie”, amesema na kuongeza kuwa
“Ili madawati haya yadumu waalimu
na wanafunzi kwa pamoja wahakikishe wanayatunza vizuri, hasa walimu
wasimamieni wanafunzi na muaelekeze namna ya kuyatunza kwakuwa hii ni
mali yetu sote”, Amesisitiza.
Aidha Dkt Nchimbi ameongeza kuwa
mkoa wa Singida uko tayari kupokea vifaa na mambo mbalimbali ya kitaifa
kutokana na kuwa katikati mwa Tanzania hivyo kuwezesha usambazaji kwa
mikoa mingine kuwa rahisi.
“Tunakaribisha taasisi,
mashirika, na hata serikali kuu kama kuna vifaa vingine leteni Singida
ni katikati na usambazaji utakuwa ni rahisi, lakini pia hata shughuli
zozote za kitaifa mkoa wa Singida uko tayari kabisa kuzipokea” amesema
Dkt Nchimbi.
Kwa upande wake Afisa Elimu Vifaa
na Takwimu wa halmashauri ya Wilaya ya Meru Frank Paul Mwambachi
amelishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kuwapatia madawati ambapo
halmashauri yake imepata madawati 400.
Mwambachi amelishukuru JWTZ kwa
kuyasogeza madawati jirani na halmashauri yake hivyo itakuwa rahisi na
salama zaidi kwake kuyasafirisha na kuyafikisha yakiwa katika hali nzuri
na kwa uharaka zaidi.
“Madawati 400 wakikaa wanafunzi
watatu watatu ina maana ni wanafunzi 1200 wamenufaika, kwakweli
tunalishukuru sana bunge kwa uzalendo wao, pia jeshi limetusaidia sana
kuyaleta madawati yetu Singida ambapo ni jirani” amesema Mwambachi.
Aidha ameongeza kuwa madawati
hayo yataboresha mazingira ya ufundishaji na ya kujifunzia hivyo
halmashauri itahakikisha wanayatunza ili wanafunzi wanufaike kwa kipindi
kirefu.
No comments :
Post a Comment