Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina (kulia) akionyesha
jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema wakati wa ziara yake
aliyoifanya mapema hii leo jijini Dar es salaam ya kukagua uchafuzi wa
mazingira katika Dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo Wilaya ya ILala.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina (kulia) akiwa
ameambatana na Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita (kushoto)
wakati wa ziara ya kukagua uchafuzi wa mazingira katika Dampo la Pugu
Kinyamwezi ambap ameipiga faini ya milioni 25 Manispaa ya Ilala kwa
uchafu wa mazingira kwa wakazi wa Pugu.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina akizumgumza na
waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo aliyoifanya katika Dampo la
Pugu Kinyamwezi lililopo Ilala jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina (kulia) akibadiishana
mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema(katikati), Sophia Mjema
na kushoto ni Meya wa jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita wakati wa
ziara ya ukaguzi wa uchafuzi wa mazingira uliofanyia katika dampo la
Pugu KInyamwezi jijini Dar es salaam.
………………………
NA; EVELYN MKOKOI
Kufuatia ziara ya Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina,
iliyofanyika Jijini Dar es Salam leo katika Manispaa ya ilala,
ilohusisha...
ukaguzi wa Dampo la Pugu Kinyamwezi, Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kupitia Mkaguzi wa Mazingira wa
kanda ya Mashariki Bw. Jaffari Chimgege, limeitoza faini Manispaa ya
jiji ya Dar es Salaam kiasi cha shilingi Milioni 25, kwa kosa la
uchafuzi wa Mazingira wa kutohudumia Dampo hilo ipasavyo na kupelekea
harufu mbaya, vumbi na maji yenye sumu kali na kuhatarisha afya ya
wakazi wa maeneo jirani viumbe hai na mzingira kwa ujumla.
Kufuatia malalamiko ya wakazi wa
mtaa wa Viwege uliyopo katika kata ya Majoe yaliyowasilishwa na
mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Bi Amina Rashid yaliyoeleza kuwa na
changamoto mbali mbali katika dampo hilo zikiwemo za vumbi na maji yenye
kemikali kwenda katika maeneo ya makazi, Naibu Waziri Mpina, ameitaka
Halmashauri ya jiji kuja na mpango mkakati utakaoweza kuupunguzia mzigo
dampo la Pugu ambalo kwa sasa linatumika kupokea takataka zote za
Halmashauri za jiji la Dar es Salaam na kuonekana kulemewa na mpango huo
uwezeshe kila manispaa kuwa na dampo lake.
Aidha Mpina alibaini kuwepo kwa
madhaifu makubwa katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kuondosha
taka katika manispaa za jiji na kuutaka uongozi wa jiji Hususan
Mkurugenzi wa Jiji kufuatilia madeni hayo kikamilifu, pamoja na kutoa deadline
ya uwasilishwaji wa fedha hizo “ni vyema ghahama za uondoshwaji wa taka
zikatokana na taka zenyewe na siyo kutoa fedha za kuhudumia taka kutoka
katika vyanzo vingine vya mapato. Alisisitiza Mpina.”
Mpina pia aliitaka manispaa ya
jiji kutafuta namna bora ya kuondosha taka sumu na kuelekeza taka zote
za matairi katika jiji la Dar es Salaam zitafutiwe sehemu tofauti na
namna pekee ya kuzitekekeza.
Akionekana kuongea kwa hasira na
msisitizo Naibu Waziri Mpina alisema, “ Hakuna kitu nisichopenda katika
utendaji wangu kama kuona taasisi za serikali zikiwa za kwanza katika
suala zima la uchafuzi wa mazingira, faini hiyo jiji mtailipa ndani ya
siku 14, na kuhakikisha mnarekebisha matobo yote yanayolalamikiwa
kupitisha maji na kupeleka katika makazi ya wananchi pamoja na kujenga
mifereji ya maji ya mvua, na maji ya sumu yaende katika mkondo sahihi wa
maji hatarishi na bila kusahau kuruhsu maji hayo baada ya kujiridhisha
na vipimo vinavyotakiwa.
Awali akitoa taarifa ya hali ya
mazingira na usimamizi wa taka katika Dampo la Pugu Kinyamwezi , Mkuu
wa Idara ya usimamizi taka wa jiji la hilo Bw. Shedrack Maximillian
alimueleza Mpina kuwa jiji linakabiliana na changamoto mbali mbali ikiwa
ni pamoja dampo kupata moto, dampo kutokuwa la kisasa na maji yenye
sumu kwenda katika makazi ya wananchi.
Hata hivyo Manispaa ya ilala
imetenga kiasi cha fedha shilingi Bilioni moja za kitanzania kwa mwaka
wa fedha ulioisha pamoja na kuzungumza na wadau wa maendeleo ikiwa ni
mkakati madhubuti wa kuweza kuboresha Dampo hilo kinalotumika kwa kiasi
kikubwa na manispaa zote za jiji la Dar es Salaam.
No comments :
Post a Comment