Ripoti ya Utalii ya mwaka 2017
iliyozinduliwa na Jumia Travel nchini Tanzania imebainisha kuwa idadi ya
watanzania wanaotumia simu katika kufanya huduma za hoteli kwa njia ya
mtandao imeongezeka na kufikia takribani asilimia 60.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwishoni mwa
wiki iliyopita imebainisha kuwa mpaka kufikia mwaka 2016 watumiaji wa
intaneti walikuwa ni zaidi ya milioni 19 kutoka milioni 17 ilivyokuwa
mwaka 2015.
Ongezeko hilo limechochewa kwa kiasi
kikubwa na kukua na kuenea kwa matumizi ya intaneti nchini (takribani
asilimia 40 ya watanzania wamefikiwa na intaneti nchini kote) lakini pia
maendeleo ya kasi kwenye sekta ya mawasiliano ya simu ambapo mpaka hivi
sasa watanzania zaidi ya milioni 40 wanatumia huduma za simu za mkononi.
sasa watanzania zaidi ya milioni 40 wanatumia huduma za simu za mkononi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti
hiyo Meneja Mkaazi wa kampuni hiyo inayojishughulisha na hudumza za
hoteli na usafiri barani Afrika, Bi. Fatema Dharsee amesema kuwa kukua
kwa sekta hiyo ni ishara nzuri kwa maendeleo ya huduma mbalimbali kwa
njia ya mtandao.
“Hakuna anayeweza kubisha kwamba dunia
yote kwa sasa imehamia mtandaoni kwani ndiko kwenye urahisi na unafuu
mkubwa. Inatia hamasa kuona kuwa watanzania nao hawako nyuma katika
kuyapokea na kuendana na mabadiliko hayo. Hivi sasa karibu kila
mtanzania ana simu ya mkononi tena ya kisasa ambayo ina uwezo wa kutumia
intaneti. Lakini cha kuvutia zaidi ni kwamba kwa namna gani watu
wanavyoutumia mtandao huu kwa manufaa yao zaidi badala ya kufanya mambo
hayana tija kwao,” alisema Bi. Dharsee.
“Jumia Travel katika ripoti yetu
tuliyoiwasilisha inaonyesha kwamba watanzania wanautumia vizuri mtandao
wa intaneti kupitia simu zao za mkononi kwenye kufanya huduma zetu. Hii
inamaanisha kwamba wameweza kugundua faida zinazotokana na wao kufanya
hivyo badala ya kwenda moja kwa moja mahotelini kuulizia huduma. Kupitia
mtandao wetu mteja anaweza kujionea huduma za mahoteli zaidi ya 1000
ndani ya wakati mfupi na kuchagulia ile inayomfaa sehemu yoyote ya
Tanzania. Kwa kuongezea, ripoti yetu imebainisha kuwa miongoni mwa
huduma zinazouliziwa sana na wateja pindi wanapoulizia hoteli ya kwenda
ni upatikanaji wa mtandao wa intaneti. Hivyo basi hii ni fursa kubwa kwa
watoa huduma kuhakikisha kuwa huduma hii inapatikana kwa uhakika na
kuboreshwa zaidi,” alimalizia Bi. Dharsee.
Hii ni mara ya pili kwa Jumia Travel
kuwasilisha Ripoti ya Utalii nchini Tanzania ambapo mwaka 2016 walifanya
hivyo pia. Miongoni mwa mambo yaliwekwa wazi na ripoti hiyo ni
kuendelea kwa kufanya vizuri kwa sekta hiyo kwani mapato yake
yameongozeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.9 mwaka 2015 na kufikia
2.1 mwaka 2016. Kiasi hiko kimechangia Dola za Kimarekani bilioni 4.6
mwaka 2016 kutokea 4.2 za mwaka 2015 katika pato la taifa.
Kwa upande wa ajira, katika mwaka 2016
sekta hiyo imeajiri watanzania zaidi ya milioni 1.3 (asilimia 11.6).
Idadi hiyo inatarajiwa kukua kwa asilimia 4.6 ndani yam waka huu wa 2017
na kufikia zaidi ya milioni 1.4. Hivyo kuifanya mojawapo ya sekta
muhimu katika uchangiaji wa uchumi na pato la taifa kwa ujumla.
Mbali na kuwasilisha ripoti hiyo, Jumia
iliwashirikisha habari njema watanzania kuwa inasherehekea miaka mitano
tangu kuanza kufanya shughuli zake barani Afrika kwa kuwarahisishia
waafrika huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.
Jumia ambayo inaundwa na kampuni tano
(Jumia Travel, Jumia Food, Jumia Market, Jumia Deals na Classified
pamoja na Jumia Jobs) pia imeujulisha umma kuwa imefanikiwa kuingia
kwenye orodha ya makampuni 50 yanayotoa huduma za mtandaoni duniani kwa
mara ya pili mfululizo.
Orodha hiyo ilitolewa na Taasisi ya
Kiteknolojia ya Massachusetts (MIT) ya nchini Marekani ambayo huyatambua
makampuni 50, yaliyopo tayari na yanayochipukia katika kutengeneza
fursa kwa kutumia teknolojia mpya kwenye kutoa suluhu na kukidhi
mahitaji ya masoko mbalimbali duniani.
Mwaka huu 2017, Jumia imeshika nafasi ya
44 ukilinganisha na ya 47 kwa mwaka 2016, ikiwa imetajwa kama kampuni
iliyojikita zaidi kutatua changamoto zinatokana na huduma kwa njia ya
mtandao barani Afrika. Changamoto hizo ni pamoja na barabara
zisizopitika kwa urahisi, tabia zisizotabirika za wateja, kukosekana
ueneaji wa kutosha wa mtandao wa intaneti ambapo kitakwimu ueneaji wake
ni asilimia 27 tu barani kote.


No comments :
Post a Comment