Wednesday, May 10, 2017

UVUNAJI WA MAZAO YA MISITU UZINGATIE SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA NCHI



NA BEATRICE LYIMO- MAELEZO
RASILIMALI ya misitu ina umuhimu mkubwa katika suala la uhifadhi wa mazingira na takribani asilimia 95 ya nishati inayotumika nchini hutokana na mimea iliyopo katika misitu.
Tanzania ina takriban hekta milioni 48 za misitu na misitu matajiwazi, zikiwemo hekta milioni 28.0 za hifadhi ya maji, ardhi na bioanuai za misitu liyohifadhiwa kwa ajili ya uvunaji na iliyopo kwenye maeneo ambayo hayajahifadhiwa kisheria.
Pamoja na umuhimu wake katika kuchangia pato la taifa na uhifadhi wa mazingira, baadhi ya misitu iliyohifadhiwa na isiyohifadhiwa inaendelea kuvamiwa kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo,  makazi, uvunaji holela wa mazao mbalimbali na uchomaji moto.
Kasi kubwa ya uvunaji wa miti kwa ajili ya magogo, mbao, nguzo na mkaa katika  mikoa mingi nchini, inaashiria uharibifu mkubwa wa mazingira na kupotea na kupungua thamani  kwa rasilimali ya misitu, hivyo kupoteza faida zitokanazo na kuwepo kwa rasilimali hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa ongezeko la ujazo wa miti kwa mwaka katika misitu nchini yote ni meta za ujazo milioni  84, ambazo ndizo zinazoruhusiwa kuvunwa kutoka katika misitu ya uzalishaji.
Matumizi ya miti katika  mwaka 2013 yalikadiriwa kufikia meta za ujazo milioni 103.5, hivyo kuwa na upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5, upungufu huo wa mahitaji au uvunaji wa ziada ya kinachoruhusiwa kuvunwa kwa mwaka ni kichochezi cha uharibifu katika misitu iliyohifadhiwa.
Inaelezwa kuwa rasilimali za misitu kuchangia asilimia 2 hadi 3 katika pato la Taifa, sambamba na shughuli mbalimbali zinazofanywa katika maeneo ya misitu kuchangia kupunguza umaskini miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kwenye shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, Wizara ya Maliasili na Utalii ilidhibiti  uvunaji wa baadhi ya miti au baadhi ya mazao ya misitu katika vipindi tofauti kwenye miaka kati ya 1995 na 2000 kwa lengo la kutathmini rasilimali iliyopo.
Kutokana na tathmini hizo, Mwongozo wa Uvunaji endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu wa kwanza uliandaliwa mwaka 2007 ili kuandaa utaratibu madhubuti katika kusimamia uvunaji na biashara ya mazao ya misitu sambamba na na kuimarisha usimamizi wa rasilimali ya misitu ya asili.
Ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu za uvunaji wa mazao hayo ulipelekea Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupinga usafirishaji wa mazao hayo ikiwemo biashara ya mkaa.
Aidha zuio hilo linakwenda sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa, pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini na vijijini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, anasema uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya maduhuli stahiki ya rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.
“Moja ya Jukumu la TFS, ni kuhakikisha inaanzisha na kusimamia rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni kosa kuvuna hovyo misitu na bidhaa zake bila kibali” anaeleza Prof. Silayo.
Prof. Silayo anaeleza kuwa, kila zao linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru stahiki na kukatiwa risiti, hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia mbalimbali zinazokatazwa ni kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.
“Tunataka kuhakikisha maduhuli ya mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata matumizi endelevu ya rasilimali za misitu hivyo  biashara hii ya miti, mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe wazi” alifafanua Prof. Silayo.
Aidha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii alisema nchi inageuka jangwa kutokana na misitu mingi kukatwa kiholela huku maduhuli ya serikali yakipotea.
Hivyo kwa kauli hiyo kila mwananchi au mhusika wa uvunaji na biashara ya mazao ya misitu nchini yampasa kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu ili kuweza kunusuru nchi kuwa jangwa.
Mbali na hayo,utaratibu wa kuomba na kupata kibali, Usajili na Leseni kwa kila atakayetaka kuvuna mazao ya misitu atatakiwa kupata barua yenye idhini ya Serikali ya Kijiji baada ya kujadiliwa na kukubaliwa na Halmashauri ya Kijiji.
Kila mtanzania anapaswa kuwa mlinzi na msimamizi wa rasilimali hizi tulizojaaliwa kwa lengo la kuweza kutunza rasilimali hizo na pia kuhakikisha maduhuli ya Serikali hayapotei.

No comments :

Post a Comment