NA MWANDISHI WETU, MANYARA
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.Dkt. Joel Bendera, (pichani juu) ameiomba
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwenda kuwekeza mkoani humo kwa
kuwapatia kuwapatia mikopo na mahitaji mengine kwa ajili ya kuongeza tija kwa
wakulima wa mkoa huo.
Akizungumza wakati wa mazungumzo na ugeni kutoka TADB
uliomtembelea Ofisini kwake, Mhe. Bendera amesema mkoa wa Manyara una fursa
nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo kulinganisha na mikoa
mingini nchini.
“Mkoa wa Manyara una fursa nyingi sana ambazo Benki
inaweza kutoa mikopo ambayo nina uhakika itarudishwa kwa wakati kwa sababu watu
wa Manyara ni waaminifu sana,” alisema Mhe. Bendera.
Akizungumza na Mhe. Bendera, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya
wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo
na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw. Assenga ameongeza kuwa sekta za kilimo na mifugo
ni sekta za kipaumbele ambazo zinazopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa
thamani mazao na mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa sekta
hizo nchini.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza
uongezaji wa thamani wa sekta hizo ili kuongeza tija sekta hizo.
“Benki inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya
Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2
hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka
Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika
kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha
kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na
kupunguza umaskini,” aliongeza.
TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa
ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya
maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na
mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara
za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti
magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao
ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mhe. Dkt. Bendera akiwakaribisha viongozi wa TDA ofisini kwake
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) akitambulisha mikopo
na huduma zinazotolewa na Benki yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Dkt. Joel
Bendera (kulia).
Mrajis Msaidizi
wa Mkoa wa Manyara, Bw. Venance Msafiri (kulia) akimtambulisha Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Mhe. Dkt. Joel Bendera (katikati).
Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa
Mkoa wa Manyara, Mhe. Dkt. Joel Bendera wakati akisisitiza umuhimu wa TADB kuwekeza
mkoani Manyara.
Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga akisisitiza utayari wa Benki yake
kuwekeza mkoani Manyara.
No comments :
Post a Comment