Wednesday, May 31, 2017

MBUGA ZA WANYAMA UNAZOWEZA KUTEMBELEA BURE WIKENDI HII

     Na Jumia Travel Tanzania

Siku ya Jumatatu ya Juni 5 itakuwa ni maadhimisho ya ‘Siku ya Mazingira Duniani’ ambayo huadhimishwa na mataifa tofauti duniani ikiwa imebeba kauli mbiu ya ‘Kuwaunganisha Watu na Mazingira Asilia.’
 Mapema wiki hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mh. January Makamba alitoa taarifa kwa umma kuwa kwa hapa nchini maadhimisho ya siku hiyo kitaifa yatafanyika kijijini Butiama mkoani Mara, mahali alipozaliwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere, ikiwa ni kuenzi jitihada zake za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Katika kunogesha sherehe hizo Waziri huyo amesema kuwa serikali imetoa ofa kwa wananchi kutembelea hifadhi yoyote ya mbuga ya wanyama bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu, kuanzia Ijumaa ya Juni 2 mpaka Jumapili ya Juni 4. Alisema kuwa lengo kubwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa mazingira yanahitaji kulindwa zaidi na zaidi.
Kauli hiyo ya Waziri imekuja siku chache baada ya kampuni inayojihusisha na masuala ya huduma za hoteli mtandaoni barani Afrika, Jumia Travel kuzindua kampeni ya ‘DemocratizeTravel’ inayolenga kuwakomboa waafrika na watanzania kiujumla katika kusafiri na kutalii vivutio mbalimbali nchini huku wao wakirahisisha huduma za malazi na hoteli.

Kampuni hiyo inalenga kuhamasisha na kutoa elimu juu ya dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi ya kwamba mchakato mzima unaohusisha utalii ni gharama. 


Katika kulifanikisha hilo kampuni hiyo imedhamiria kuelimisha juu ya vivutio vilivyopo nchini, masuala ya msingi ya kuzingatia wakati wa kusafiri pamoja na kurahisisha gharama za malazi kupitia hoteli za kila hadhi zilizopo kwenye mtandao wao wa travel.jumia.com.   
Baadhi ya changamoto zilizopo ni pamoja na mwamko mdogo wa watanzania kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo karibu na wanayoishi. Wapo baadhi yao hawafahamu kuwa wanaishi na vivutio hivyo na wengine huchukulia mchakato mzima unahusisha gharama kubwa.

No comments :

Post a Comment